Madiwani kwa Lowassa wasusa.....Kata zao zakosa Wagombea, Wasema Wanasubiri Tamko la Lowassa - MULO ENTERTAINER

Latest

17 Jul 2015

Madiwani kwa Lowassa wasusa.....Kata zao zakosa Wagombea, Wasema Wanasubiri Tamko la Lowassa

Kasi ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuomba nafasi za udiwani na ubunge katika Jimbo la Monduli, inasuasua na tayari chama hicho kimeitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Siasa kitakachokutana leo kukuna vichwa kutafuta ufumbuzi wa hali hiyo.

Katibu wa CCM Wilaya ya Monduli, Elisante Kimaro, alisema jana kuwa kusuasua kwa wanachama kuchukua fomu za kuomba kugombea nafasi hizo kunatokana na kushuka kwa morali ya wanachama baada ya Mbunge wa zamani, Edward Lowassa, aliyekuwa akiwania kuteuliwa na chama chake kugombea urais, kukatwa jina lake.

“Zoezi la uchukuaji wa fomu za udiwani linasuasua, lilianza juzi na siku ya mwisho ni Julai 19, mwaka huu saa 10 jioni.

“Zoezi hili ni gumu sana, hata hivyo bado ni mapema sana kutoa taarifa, lakini morali ya wanachama kuchukua fomu za kuomba kugombea imepungua,” alisema.

Alisema ameitisha kikao cha dharura cha Kamati ya Siasa chenye wajumbe 16 kuzungumzia suala hilo ili kwa pamoja wahamasishe wanachama kugombea.

“Tunawahimiza wanachama wajitokeze kuchukua fomu za kugombea nafasi hizo,” alisema na kuongeza: “Hili jimbo ni ngome ya CCM na wala sina shaka na hilo.”

Alisema kusuasua huko kunatokana na baadhi ya madiwani waliomaliza muda wao kufanya propaganda ya kuwazuia wanachama kwenda kuchukua fomu kwa madai kwamba wasubiri kwanza kauli ya mbunge wao.

“Baadhi ya madiwani wa zamani wanatengeneza propaganda, hawa ni madiwani wale ambao hawakubaliki katika kata zao…wanawahamasisha watu wasichukue fomu kwa kigezo kwamba wasubiri kauli ya Mbunge Lowassa, jambo ambalo siyo kweli," alisema.

Aliongeza: “Lowassa hajawahi kufanya kitu kama hicho cha kuwaambia wanachama wasichukue fomu hadi atakapotoa kauli yake…jana (juzi), alikuja hapa Monduli kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, hakutamka lolote, alisema tu hana la kusema.”

Alisema watu hao wanatumia mgongo wa Lowassa kueneza propaganda.

Alisema kwa upande wa ubunge hadi sasa amejitokeza mwanachama mmoja tu, Mbayani Tayayi, aliyechukua fomu yake jana saa 4:00 asubuhi, wakati kwa upande wa udiwani waliochukua fomu ni mwanachama mmoja mmoja katika kata za Mswakini, Lepurko na Engutoto.

Pamoja na kusuasua huko, Kimaro alisema atahakikisha kata zote 20 zinapata wagombea wa udiwani na kumpata mgombea ubunge.

Alizitaja kata hizo kuwa Engaruka, Engutoto, Esilalei, Lepurko, Loksale, Majengo, Makuyuni, Meserani, Nalalani, Lemooti, Moita, Monduli Juu, Monduli Mjini, Mfereji, Mswakini, Mto wa Mbu, Migungani, Selela, Sepeko na Lashaini.

Alisema tangu kumalizika kwa mchakato kupata mgombea ndani ya chama hicho Julai 12, mwaka huu, mjini Dodoma ambapo jina la Lowassa lilikatwa katika mazingira ya kutatanisha, kumekuwa na maneno mengi yakisambaa kwenye mitandano ya kijamii kwamba Lowassa anakihama chama hicho.

“Hizi habari si za kweli, bado tuna imani na Lowassa,” alisema.

Alisema mchakato wa kumpata mgombea ndani ya chama hicho tayari umemalizika kwa kumpata mgombea wake, Dk. John Magufuli.

Hali ilivyo:
Baadhi ya wakazi mjini Monduli walisema kitendo cha kuenguliwa kwa mbunge wake katika kinyang’anyiro cha urais, kimewavunja moyo kwa maelezo kuwa utaratibu haukufanyika kwa haki.

Walisema wanahamasishana kuwapigia kura wagombea watakaosimamishwa na vyama vya upinzani wakidai CCM imefia mikononi mwa Mwenyekiti wao wa Taifa.

Katika kituo cha mabasi cha Monduli, wapiga debe walikuwa wakiwataka abiria ambao ni wanachama wa Chadema kuingia daladala za Arusha zilizopo kituoni hapo huku wakiwataka abiria ambao ni wanachama wa CCM kwenda kusubiri magari yao (mashangingi) yaliyopo eneo la CCM.

Wiki iliyopita, CCM walifanya vikao vya uteuzi wa mgombea wao.

Chama hicho kilimteua Dk. John Magufuli kwa asilimia 87.1 na Samia Suluhu Hassan, kuwa mgombea mwenza ili kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.