Sumaye Atoa Siri ya Kuibana CCM....Akana Kumwita Lowassa Fisadi - MULO ENTERTAINER

Latest

21 Sept 2015

Sumaye Atoa Siri ya Kuibana CCM....Akana Kumwita Lowassa Fisadi

Waziri Mkuu Mstaafu wa awamu ya tatu, Fedrick Sumaye amesema kama Uchaguzi Mkuu wa Oktoba utakuwa huru na haki, basi umoja wa vyama vinavyounda Ukawa watashinda na kuingia madarakani.

Sumaye amesema ana uhakika kwa asilimia kubwa upinzani wana nafasi kubwa ya kushinda Katina uchaguzi mkuu ujao ni ndio sababu mojawapo iliyomfanya ajitoe CCM na kujiunga upinzani.
Akihojiwa katika kipindi cha Funguka kilichorushwa na kituo cha televisheni cha Azam Tv, Sumaye ambaye alikuwa waziri mkuu kwa miaka kumi katika serikali ya awamu ya tatu amesema amejitoa CCM kwa sababu ameona hali ndani ya chama hicho si nzuri na kuwa kuna nafasi kubwa ya upinzani kuingia madrakani.

Sumaye alisema hajajiunga na upinzani kwa kuahidiwa madaraka yoyote na kwamba lengo kubwa ni kutoa ushauri kwani anaamini ana uzoefu mkubwa wa kuitawala na atakuwa msaada kwao.
Akizungumzia kuhusu ufisadi ambapo awali alikaririwa akisema atatoka CCM endapo chama hicho kitamchagua fisadi, Sumaye alisema hana tatizo na Dk Magufuli lakini mfumo mzima wa chama na kuongeza kuwa hajawahi mahali popote kumtaja kwa jina Lowassa kuwa ni fisadi.
“Vita yangu ya ufisadi nimeanza maisha yangu yote na hakuna mahali popote nimewahi kumtaja Lowassa kuwa ni fisadi, taarifa ya Bunge haijawahi mtaja Lowassa kushiriki jinai yoyote katika suala la Richmond,” alisema Sumaye.

Kuhusu umiliki wa ardhi kubwa huku wananchi wengi wakilia hawana ardhi, Sumaye alisema haoni tatizo lolote kumiliki ardhi kihalali huku akisema eneo la hekari 300 analomiliki ni kidogo ikilinganishwa na vigogo wengine.
“Kama ukitupanga viongozi na kuangalia ukubwa wa mashamba tuliyonayo, mimi nitakuwa mkiani,” alisema Sumaye na kuongeza:

“Hivi kuwa na shamba ni dhambi? Nchi yeyote inayoendelea, watu ambao watabaki kwenye kilimo watakuwa na ardhi kubwa.”
Sumaye aliongeza kusema kuwa hata kama Ukawa hawataingia madarakani, hatarudi tena CCM na ataendeleza upinzani.