Dk Reginald Akana Kujitoa kwa Lowassa...Asema Haya Kuhusu Taarifa zilizoenea Mtandaoni - MULO ENTERTAINER

Latest

12 Oct 2015

Dk Reginald Akana Kujitoa kwa Lowassa...Asema Haya Kuhusu Taarifa zilizoenea Mtandaoni

MWENYEKITI Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Dk Reginald Mengi amesema kuwa taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa yeye amejitoa kwa Lowasa si za kweli.

Alisema hayo kwa waandishi wa habari, aliokutana nao jijini Dar es Salaam, jana.

Alikutana na waandishi hao ili kufafanua kuhusu taarifa, aliyosema inaenezwa kupitia mitandao ya kijamii, yenye kichwa cha habari ‘Mengi ajitoa rasmi kwa Lowassa’. Edward Lowassa ni mgombea urais wa Chadema anayeungwa mkono na vyama vinavyounda Ukawa.

Mbali na Chadema, vyama vingine katika Ukawa ni CUF, NCCR-Mageuzi na NLD.

Taarifa yake aliyosoma kwa waandishi wa habari kuhusu suala hilo ilisema: “Nimeomba tukutane leo kwa jambo moja tu. Kuwafahamisha kwamba taarifa inayoenezwa kupitia mitandao ya kijamii yenye kichwa cha habari kinachosema ‘Mengi ajitoa rasmi kwa Lowassa’ na eti nimesema ‘kama hawa jamaa (Ukawa) watashinda nafasi ya Urais, basi ni baada ya miaka 10 siyo hivi sasa,” alisema.

Dk Mengi alisema “Taarifa hiyo ni ya uongo, upotoshaji na uchochezi”. Dk Mengi alieleza kuwa “Taarifa za aina hii zisipokemewa na kuchukuliwa hatua za haraka, zitaathiri amani ya Taifa letu. Ni matarajio yangu kwamba vyombo husika vitachukua hatua zinazostahili kwa haraka iwezekanavyo”.