Majaribio mabasi ya mwendo kasi mbioni kuanza - MULO ENTERTAINER

Latest

23 Mar 2016

Majaribio mabasi ya mwendo kasi mbioni kuanza


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema mabasi yaendayo haraka (DART) yataanza kufanyiwa majaribio ndani ya wiki moja kuanzia sasa ili madereva waanze kuzoea njia na taa za kuongozea magari.
“Wataanza na mabasi kati ya 30 – 50 ambayo yatapita kwenye njia zote za mradi huo. Zoezi hilo litafanyika ili watumiaji wengine wakiwemo waendesha daladala, bodaboda na watembea kwa miguu waweze kutambua kuwa njia ya mabasi yaendayo kasi si ya kwao, hivyo waanze kuzoea,” alisema.
Alitoa kauli hiyo jana wakati alipofanya ziara ya ghafla katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri, Dar es Salaam iliyokuwa na lengo la kuangalia mfumo wa majiko ya gesi sokoni hapo na kukagua ujenzi wa ukuta unaotenganisha soko hilo na mabasi yaendayo kasi.
Waziri Mkuu ambaye ametembelea soko hilo kuanzia saa 5:10 hadi saa 5:54, alitoa maelezo hayo wakati akijibu maombi ya mfanyabiashara mmoja, Sharifu Ramadhani ambaye alisema wanatumia fedha nyingi kwa ajili ya usafiri kwa vile mabasi mengi yanaishia Mnazi Mmoja.
“Mabasi yanaishia Mnazi Mmoja na huku ni mbali kwa hiyo tunalazimika kutembea kwa miguu kwa sababu kukodi teksi ni gharama kubwa,” alisema Ramadhani.
Akifafanua kuhusu hatua iliyofikiwa kwenye utekelezaji wa mradi huo, Waziri Mkuu alisema: “Hivi sasa wanakamilisha ufungaji wa mitambo ya kukatia tiketi ambapo abiria atakuwa na kadi kama za benki ambayo anaijaza fedha halafu anapita kwenye mashine, kiasi cha nauli kinakatwa halafu anaingia kwenye basi, hakutakuwa na muda wa kukata tiketi.”