Imefichuka Sehemu Alipo Dereva wa Tundu Lissu...Hayupo Tanzania..Mbowe Ataja Alipo - MULO ENTERTAINER

Latest

10 Sept 2017

Imefichuka Sehemu Alipo Dereva wa Tundu Lissu...Hayupo Tanzania..Mbowe Ataja Alipo

Mwenyekiti wa (CHADEMA) Freeman Mbowe amefunguka na kuweka wazi sehemu alipo dereva wa Tundu Lissu ndugu Simon Mohamed Bakari na kusema kwa sasa yupo nchini Kenya akipatiwa huduma za kisaikolojia kufuatia kushuhudia tukio hilo la kinyama.

Mbowe amesema hayo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari ambapo ameweza kuzungumzia mambo mbalimbali kuhusu sakata hilo na kusema kuwa waliona ni busara kumchukua dereva huyo na kuwa naye nchini Kenya kwa ajili ya kupatiwa msaada huo hadi watakapooona hali yake ya kiafya na uhakika na usalama wake ndiyo anaweza kurejea nchini Tanzania.

"Dereva wa Mhe. Lissu, Simon Mohamed Bakari naye tunaye hapa Nairobi akiendelea kupata huduma za kisaikolojia. Alishuhudia shambulio lile na aliokoka kimiujiza. Anasumbuliwa na msongo mkubwa wa mawazo. Naye hatukuona busara kuendelea kumwacha nchini hadi hapo hali yake ya kiafya na kiusalama itakapohakikishwa. Ni dhahiri kwa aina ya shambulio lilivyokuwa, wauaji walikusudia kuwauwa wote, Mhe. Lissu na hata Dereva wake" alisema Freeman Mbowe

Mbali na hilo Mbowe amewataka wabunge wa upinzani kuwa na tahadhari kubwa akidai kuwa kama wasipokuwa makini huenda kiongozi mwingine anaweza kupata matatizo kama hayo hata hivyo amesema kuwa tamko la chama chake litakuja karibuni.

"Tutamuenzi Baba wa Taifa aliyetuasa: “tukiwa waoga tutatawaliwa ma madikteta!” Wabunge na Viongozi wa Upinzani ndiyo “Target”. Nawasihi viongozi na wabunge wetu wachukue kila tahadhari. Wanachama nao wawe tayari kulinda na kupigania wajibu wetu, usalama wa viongozi na chama chetu kwa ujasiri. Tusipochukua hatua, kesho atadhurika mwingine!Tamko na agizo rasmi la Chama litafuata karibuni" alisema Freeman Mbowe.

Freman Mbowe amedai kuwa Tanzania si sehemu salama tangu umefanyika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015 na kudai kuanzia hapo yalianza kujitokeza kwa mauaji ya viongozi kikiwepo kifo cha Mhe. Alphonce Mawazo Mkoani Geita, Kupotea kwa kina Ben Saanane. Kutekwa  wasanii na kufanyiwa mateso makubwa pamoja na Wabunge kufungwa na kushtakiwa kila siku.