Babu Tale Atiwa Mbaroni kwa Amri ya Mahakama - MULO ENTERTAINER

Latest

23 May 2018

Babu Tale Atiwa Mbaroni kwa Amri ya Mahakama

Babu Tale Atiwa Mbaroi kwa Amri ya Mahakama
Mkurugenzi wa Kampuni ya Tip Top Connection ya jijini Dar es Salaam,  Hamis Taletale maarufu Babu Tale, ametiwa  mbaroni na kufikishwa mahakamani na Jeshi la Polisi Kanda Maalum Dar es Salaam kwa amri ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es  Salaam.

Babu Tale amekamatwa kufuatia amri iliyotolewa Februari 16, 2018 na Naibu Msajili wa Mahakama  Kuu Kanda Maalum, Wilbard Mashauri iliyoelekeza kukamatwa mtuhumiwa huyo na ndugu yake, Idd Taletale.

Amri hiyo pia, ilielekeza watakapokamatwa wapelekwe Gereza la Ukonga wakiwa wafungwa wa kesi ya madai, hadi hapo mahakama hiyo itakapotoa maelekezo mengine.

Hata hivyo, Babu Tale hakuweza kupatikana na ndipo mahakama hiyo ikatoa amri nyingine kama hiyo Aprili 4 mwaka huu. Tangu hapo wamekuwa wakitafutwa bila mafanikio hadi jana alipokamatwa.

Mahakama hiyo iliwaamuru kumlipa Mhadhiri wa Dini ya Kiislamu, Sheikh Hashim Mbonde kiasi cha Sh250 milioni, baada ya kupatikana na makosa ya ukiukwaji wa haki za hakimiliki kwa kutumia masomo yake kibiashara bila ridhaa yake kinyume cha Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki.

Baada ya kutiwa mbaroni leo alifikishwa mahakamani saa tisa alasiri  kwa ajili ya hatua zaidi. Hata hivyo,  Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, aliyetoa amri ya kumkamata hakuwepo.  Kufuatia kutokuwepo kwa msajili huyo Taletale amerudishwa mahabusu Kituo Kikuu cha Polisi hadi kesho asubuhi atakapopelekwa tena mahakamani hapo kwa hatua zaidi.

Hukumu hiyo iliyomwamuru Babu Tale na nduguye kulipa kiasi hicho cha fedha,  ilitolewa na Jaji Agustine Shangwa, Februari 18,2016  katika kesi ya madai namba 185 ya mwaka 2013, iliyofunguliwa na Sheikh Mbonde kutokana akiwalalamikia ndugu hao kutumia mahubiri yake kibiashara bila ridhaa yake.