Wakazi wa Mkoa wa Lindi wametakiwa kushikamana ili kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo yao na nchi. - MULO ENTERTAINER

Latest

28 Dec 2014

Wakazi wa Mkoa wa Lindi wametakiwa kushikamana ili kufanya kazi kwa bidii ili kuleta maendeleo yao na nchi.

WAKAZI wa mkoa wa Lindi wametakiwa kushikamana kwa pamoja, kufanya kazi kwa bidii na kuzitumia rasilimali zilizopo ili kujiletea maendeleo. Rai hiyo imetolewa jana Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wilaya ya Lindi
mjini Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Mitwero Stendi Kata ya Rasibura wilayani humo.
Mama Kikwete ambaye ni Mke wa Rais Dk. Jakaya Kikwete alisema mkoa wa Lindi umejaliwa kuwa na rasilimali nyingi ikiwa ni pamoja na zao la korosho, ardhi yenye rutuba, bahari na gesi lakini bado kuna changamoto zinazowakabili wananchi na hivyo kukwamisha maendeleo yao. Alizitaja changamoto hizo kuwa ni pamoja na elimu kwani baadhi ya wanafunzi wafikapo darasa la tano wanaacha shule kwa ajili ya utoro, mimba za utotoni na vijana kutokufanya kazi kwa bidii.
“Kuna baadhi ya watoto wakifika darasa la tano wanaanza tabia ya utoro hakikisheni wanakwenda shule kusoma kwani elimu itawasaidia katika maisha yao, msikubali waache shule. Kutokana na umri wao mdogo wanaona raha kuacha shule na kwenda kucheza lakini wakifika umri wa utu uzima ndiyo watakapoona umuhimu wa elimu,” 
“Maisha bora kwa kila mtanzania yanawezekana ikiwa kila mtu atapata elimu itakayomsaidia katika maisha yake, wakati shule za Sekondari za Kata zinajengwa kuna baadhi ya watu walitubeza na kuziita majina ya ajabu ikiwa ni pamoja na shule za Yeboyebo lakini shule hizi zimewasaidia watoto wengi kutoka familia maskini ambao wameweza kupata elimu,” alisema Mama Kikwete. 
Kuhusu tazizo la mimba za utotoni alisema ni hatari kwa maisha ya Mama na mtoto lakini kama kijana atasoma mimba zitaepukika, jukumu la wananchi ni kuhakikisha watoto wao wanasoma kwa bidii na kutokubali kupewa mimba ambazo zitawakatisha masomo. 
Kwa upande wa vijana MNEC huyo aliwahimiza kuangalia mstakabali wa maisha yao na kutumia muda wao kufanya kazi kwa bidii kwa kufanya hivyo watapata maendeleo kwani hizi sasa kuna baadhi ya vijana wakati wa asubuhi wanaacha kwenda shamba kulima na kucheza Pool kwa kufanya hivyo ni vigumu kupata maendeleo. 
“Vijana wengine wanatumia madawa ya kulevya na kuvuta sigara wanajua kwa kufanya hivyo ndiyo ujanja kitendo ambacho siyo ukweli, bali unaharibu afya yako na kujirudisha nyuma kimaendeleo. Kama wewe kijana unahitaji kuwa na maisha bora ni lazima uachane na vitendo hivyo na kufanya kazi,” alisisitiza.  
Licha ya kufanya mkutano huo wa hadhara Mama Kikwete pia alifanya vikao na wajumbe wa Halmashauri kuu ya CCM matawi ya Mbanja, Mabano na Mitwero Stendi na kuwataka wajumbe hao kuwapa vijana nafasi za uongozi pale watakapojitokeza kugombea nafasi hizo. Pia aliwahimiza wajumbe hao wakiwemo vijana, wanawake na wanaume kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika hapo mwakani ili kuwe na ushindani wa kutosha ndani ya chama. Mama Kikwete yupo wilayani humo kwa ajili ya shughuli za kichama na katika mkutano wa hadhara aligawa kadi kwa wanachama wapya 23 walijiunga na Chama Cha Mapinduzi.