KIBA KUMBUKA MAJIVUNO, MARINGO NDIVYO VILIVYOKUPOTEZA! - MULO ENTERTAINER

Latest

10 Mar 2015

KIBA KUMBUKA MAJIVUNO, MARINGO NDIVYO VILIVYOKUPOTEZA!


Kwako
staa uliyerudi kivingine na wimbo wa Mwana, Ali Kiba. Vipi uko poa? Bila shaka u-mzima wa afya na unaendelea na harakati zako za kimuziki.Ukitaka kujua hali yangu, mimi ni mzima wa afya namshukuru Mungu maisha yanasonga. Naendelea na majukumu ya kila siku likiwemo hili la kukuandikia barua.
Pasipo kupepesa macho, pamoja na salamu, dhumuni la kukuandikia barua hii ni kwamba kuna kitu kimenigusa nataka kukukumbusha maana akili ya mwanadamu siku zote imeumbwa kusahau.
Ni rahisi sana mtu kula msoto mkubwa lakini ndani ya dakika chache tu pale unapopata mafanikio, unasahau.Nakumbuka kabla ya kuachia nyimbo za Kimasomaso na Mwana ambazo zinaendelea kufanya vizuri hadi sasa, ulikuwa kimya. Najua unaweza usikubaliane na mimi lakini ukimya ule ulitokana na kujisahau baada ya kuwa na mafanikio makubwa.

Kipindi kile ulifanikiwa kuiteka Bongo, kila mmoja alikuwa akikutambua wewe kama namba moja hususan pale ulipofanikiwa kuwa msanii pekee kutoka Tanzania na kwenda kufanya kolabo maalum iliyoandaliwa na legendary wa muziki kutoka Marekani, R. Kelly.
Kiba ulikuwa Kiba kweli. Kipindi hicho ukitaja Diamond, kila mtu anakuuliza ndiyo nani. Hakuna aliyemjua. Kila mmoja alikujua wewe kwamba ndiyo kioo cha Tanzania katika anga za kimataifa, uwezo wako uliheshimika.
Hapo ndipo zilipoanza pozi, majivuno kama siyo maringo. Ukawa unapanga bei yoyote ya shoo hata ya kukomoa ili mradi anayeandaa shoo ashindwe kufanya kazi na wewe.
Pia hapo ndipo ulipokuwa ukitoa ushirikiano hafifu kwa mashabiki wako kwa kujitenga na vyombo vya habari.Ulijisahau ukaona jina ulilolitengeneza linaweza kuendelea kuwepo hata kama usipozungumza lolote kwa mashabiki wako kupitia vyombo vya habari.
Hata hao waandishi waliokuwa wakitaka kufanya mahojiano na wewe kwa faida yako nao ulikuwa ukiwaletea pozi.Mashabiki wakaanza kukumiss katika kazi zako. Wakawa wanakosa habari zako mpya kiasi cha kukuweka kando na kumpa sapoti bwa’mdogo ambaye sasa anakimbiza kinoma, Nasibu Abdul ‘Diamond’ (wakati huo wewe ulimuona wa kawaida sana).
Kaugonjwa ka kujisahau naona tayari kameanza kukunyemelea. Nimetonywa kwamba umeanza tena. Pozi zimeanza, ‘vurugu’ za vyombo vya habari zimeanza kukata.Nahisi zile shoo kadhaa ulizopiga zimeanza kukusahaulisha hata ile mipango yako ya kutoa video za nyimbo zako mpya tena sizisikii. Nikwambie tu, ulipata bahati Watanzania walikupokea kwa mara nyingine maana ipo mifano ya wasanii wengi waliowika wakapotea lakini kila walipotaka kurudi walichemka.
Itumie fursa ya kurudi na kukubalika upya kama fundisho kwako, usikubali kukaa mbali na mashabiki wako. Wape kazi mpya, wape habari zako kila siku ili waendelee kukupa sapoti wasije wakakusahau ukarudi kule ulikokuwa.Kwa leo ni hayo tu, asante kwa kunisoma.