MAJANGA juu ya majanga! Siku chache kufuatia kufanyiwa kipimo na kubainika kuna tatizo kwenye ubongo baada ya kupigwa chupa kichwani kwenye Klabu ya New Maisha, Masaki jijini Dar, mkali wa sinema za Bongo, Kajala Masanja ‘Kay’ amepata pigo lingine la daktari kumwambia hawezi kuzaa tena!
Kwa mujibu wa chanzo makini, Kajala alipewa maelezo hayo mapema wiki hii baada ya kufanyiwa kipimo na daktari bingwa wa hospitali moja iliyopo maeneo ya Morocco jijini Dar.
HISTORIA YA TATIZO
Kwa mujibu wa chanzo hicho, awali staa huyo alikuwa akisumbuliwa na tatizo la maumivu makali ya tumbo kwa kipindi kirefu na mara kwa mara hali iliyomlazimu kwenda kwenye hospitali mbalimbali za jijini Dar na kutibiwa lakini bila mafanikio.
“Unajua awali, aliamini amepata vidonda vya vitumbo (Ulcers).
“Pamoja na kupewa dawa mbalimbali kama ‘antibiotic’ kama Amoxicillin, Tetracycline, Clarithromycin na Metronidazole, dawa zenye uwezo wa kupunguza uzalishaji wa tindikali tumboni lakini wapi.
HALI YAZIDI KUWA MBAYA
“Kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya ndipo mwanzoni mwa wiki hii alipojisikia maumivu ya kupindukia hivyo alikwenda kwenye hospitali ile iliyopo Morocco na majibu ya vipimo yakaonesha kuwa ana uvimbe mkubwa kwenye kizazi!” Kilisema chanzo hicho.
Mnyetishaji wetu alidai kuwa, daktari huyo alimshauri kufanyiwa upasuaji wa haraka ili kuondoa uvimbe huo kwa sababu anaweza pia kunyemelewa na tatizo la kansa achilia mbali ishu ya kutozaa tena.
KAJALA AISHIWA NGUVU
“Yaani Kajala aliishiwa nguvu kabisa alipoambiwa maneno hayo na kujikuta akimwaga machozi,” kilisema chanzo hicho.
KAJALA ASAKWA KUTHIBITISHA
Baada ya gazeti hili kupata habari hiyo, lilimtafuta Kajala ambapo alikiri kukutwa na tatizo hilo na ni kitu ambacho kimemchanganya sana hasa akimwangalia binti yake Paula (aliyezaa na Prodyuza wa Bongo Records, Paul Matthyasse ‘P Funk’), bado mdogo hivyo kujikuta akidondosha chozi.
“Yaani mtu akikuambia una ugonjwa kama huo, lazima uumie kwa kweli na mara nyingi namfikiria mtoto wangu bado mdogo. Kwa sasa najitahidi kufanya matibabu ya haraka ili kuondoa tatizo hilo,” alisema Kajala.
KITAALAM
Kwa mujibu wa daktari mmoja wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambaye aliomba jina kusitiriwa, mwanamke akiwa na uvimbe mkubwa kwenye mfuko wa uzazi na kwa muda mrefu, matibabu yake salama ni kukiondoa kizazi.
“Lakini kuna wanawake wanapatwa na vimbe mbalimbali kwenye mfuko wa kizazi lakini si kubwa, ni rahisi kuondoa kwa kuchubua kitaalam na kizazi kikabaki salama,” alisema daktari huyo.
WEMA BILA KUJALI
Wakati huohuo, Kajala amekumbwa na janga baada ya aliyekuwa shosti wake wa kufichiana siri kama siyo kutunziana mambo yao ya ndani, Wema Sepetu kumpaka runingani!
Baada ya Kajala kujishusha akisema yupo tayari kupatana na mwenzake, Wema, mwanadada huyo amemshukia Kajala akimwita ‘bogasi’ yaani mjinga na kwamba ni mtu mzima lakini hana akili.
Akizungumza kupitia Clouds TV Jumanne iliyopita, Wema alifunguka kwamba hivi karibuni alishangazwa na kitendo cha Kajala kuandika vitu vya ajabu kwenye ukurasa wake wa Mtandao wa Instagram akisema amejishusha kumuomba msamaha ili aonewe huruma kwa watu na yeye (Wema) aonekane kuwa hafai.Mkali wa sinema za Bongo Wema Sepetu.
“Kabla ya kuandika vile nilikuwa nipo tayari hata akija kwangu nimkaribishe nimsikilize lakini kwa sasa sitaki kuambatana na Kajala.“Kajala ni mtu mzima lakini hana akili. Kuwa na Kajala ulikuwa ni upepo tu unapita. Alichokifanya mimi namuona bogus,” alisema Wema.
Kwa upande wake, Kajala alimjibu kwa kifupi bila kutaka kubebanisha maneno kwa kusema: “Siku zote duniani ukikimbizana na chizi na wewe utaonekana chizi, nimejishusha, nimechoka.”