Millard Ayo Abanwa Kuhusu Uhusiano wake na Jokate, Lulu Michael na Wolper - MULO ENTERTAINER

Latest

25 Jun 2015

Millard Ayo Abanwa Kuhusu Uhusiano wake na Jokate, Lulu Michael na Wolper

Mtangazaji mwenye sauti nzito Bongo kupitia Clouds FM, Millard Ayo, Jumatatu iliyopita alibanwa azungumzie uhusiano wake na warembo wenye majina makubwa nchini, Jokate Mwegelo ‘Kidoti’,  Jacqueline Wolper na Elizabeth Michael ‘Lulu’ ambapo alimfungukia mmojammoja.

Katika mahojiano maalum na Kipindi cha Sporah Show, mtangazaji alimbana Millard akimtaka aseme ukweli kuhusu warembo hao ambapo  alianza kwa kumzungumzia Lulu kuwa hajawahi kuwa mpenzi wake zaidi ya kumfahamu katika sanaa.

“Kuhusu Lulu! Hapana sijawahi kabisa kuwa na uhusiano naye. Yaani hata kuwaza sijawahi. Namfahamu kuwa ni mwigizaji na ni mtu ambaye nimekuwa nikimfuatilia kupitia kazi zangu za utangazaji,” alisema mtangazaji huyo staa.

Millard aliendelea kupangua, ikafika zamu ya Wolper. Alikana vikali kuwa naye hata kujuana kwao si kwa ukaribu. Alisema:


“Haa! Wolper ndiyo kabisa, nimekuwa nikimuona na kumsikia tu, wala sikuwahi kumuwazia kwa lolote lile isipokuwa ninamjua kama msanii wa Bongo Muvi na huwa nakutana naye kama ninavyoweza kukutana na mtu mwingine yeyote ambaye hatujuani.”

Kwa upande wa Jokate, hapo alipiga kituo kidogo na kuanza kumzungumzia kwamba, amemfahamu miaka mingi na alikuwa akimpenda kama ‘girl friend’ wake kwani wakati anasoma alishawahi kupanda naye daladala na wakapiga stori.

“Nampenda Jokate kwa sababu mpole, anatoka katika familia ya wachakarikaji, hivyo nimekuwa nikimshirikisha katika mambo yangu. Nampenda kwa sababu hiyo ila huwezi kuamini, nilipotezana naye na baadaye tumekuja kukutana tayari yeye ni maarufu na sikuwahi kumwambia chochote juu ya kumpenda kwangu kwa kuwa tayari ana ‘boy friend’ wake.

“Jokate naye anamjua mchumba wangu ingawa hajawahi kumuona. Kwa sasa namchukulia kama dada yangu tu kwa kuwa hakuna popote ambapo nimewahi kutoka naye kimapenzi hata kwa dakika moja zaidi ya kuwasiliana naye kikazi. Mara kadhaa nimekuwa nikimtafuta hata kama ni usiku wa manane nikiwa na jambo na huwa sisiti kumshirikisha,” alisema Millard.

Kwa upande wa Jokate baada ya kufikishiwa taarifa ya maneno ya Millard alishangaa, akasema yeye hajui chochote. Kwanza aliwekewa mtego kama angeuingia kwa kuambiwa Millard amemtaja yeye kuwa ni mchumba wake, akashtuka na kusema:

“Huh! Kasema hivyo lini? Maana mimi sijasikia lolote na siyo kweli kama ni mpenzi wangu na sijui kwa nini kaongea hivyo. Kwa kweli sijasikia wala kuongea naye.”

Wolper yeye alipoulizwa juu ya maneno ya Millard kwamba hawajahi kuwa karibu kwa jambo lolote zaidi ya kuonana barabarani alishtuka:

“He! Ni kweli lakini. Hata mimi namwonaga tu. Hivi yupo kwani hapa Bongo? Sina koneksheni ya kitu chochote na yeye.”

Lulu alipotafutwa juzi, simu yake iliita kwa muda mrefu lakini hakupokea.

Kuhusu Millard na Jokate, baadhi ya vyombo vya habari vimewahi kuripoti kuwa wako karibu kiasi kwamba, maswali ni mengi kuliko majibu.

Kwenye ‘bethidei’ ya Millard iliyofanyika Januari 26, mwaka huu nyumbani kwake, Ubungo Msewe jijini Dar, Jokate alishiriki kwa kumpelekea keki ya ‘kumuwishi’ ambayo ilizua utata.