SERIKALIimesema itaanza kutekeleza ahadi yake ya kutoa elimu ya sekondari bure katika mwaka wa fedha 2015/16.
Taarifa hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi, Celina Kombani wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Lushoto, Henri Shekifu (CCM).
Katika swali lake, Shekifu alitaka kujua kama tangazo hilo la Serikali la kutoa elimu ya sekondari bure ni la kweli na utekelezaji wake utaanza lini.
Kombani alisema tangazo hilo ni la kweli na utekelezaji wake utaanza katika mwaka wa fedha 2015/16.
Awali akijibu swali la msingi la Mbunge wa Kibaha Mjini, Francis Koka (CCM), Kombani alisema uanzishwaji wa Mfuko wa Elimu ni wa kisheria ambao unawataka wadau mbalimbali ndani ya wilaya kuchangia mfuko na fedha zinazokusanywa zinatumika kuboresha elimu kulingana na vipaumbele vya halmashauri husika.
“Sambamba na uanzishwaji wa Mfuko wa Elimu, uboreshaji wa mfuko huo unafanyika kwa kutumia asilimia tatu ya mapato ya ndani ya halmashauri .
“Kupitia mifuko hii, imeanzishwa Mamlaka ya Elimu nchini ambako mwanachama huchangia Sh 500,000 kwa mwaka na kuweza kuomba fedha za kuboresha elimu katika maeneo ambayo wanayapa kipaumbele,” alisema.
Aliupongeza Mji wa Kibaha ambao tayari una mfuko wa elimu ambao umewezesha kupatikana kwa madawati 500 na ujenzi wa maabara katika shule za sekondari za Miembasa na Mwambisi.
Katika swali lake, Koka alitaka kujua mpango wa Serikali wa kuboresha Mifuko wa Elimu iliyoanzishwa katika halmashauri kwa lengo la kuboresha elimu.