Dk Kigwangala Apata Wakati Mgumu Kuitetea CCM Katika Mdahalo - MULO ENTERTAINER

Latest

15 Sept 2015

Dk Kigwangala Apata Wakati Mgumu Kuitetea CCM Katika Mdahalo

Mwakilishi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mdahalo wa MkikiMkiki unaohusu Uchaguzi Mkuu uliofanyika jijini Dar es Salaam, Dk Hamis Kigwangala jana alikuwa na wakati mgumu kutetea sera za chama hicho tawala katika sekta za elimu na afya.

Dk Kigwangala ambaye pia ni mgombea ubunge jimbo la Nzega Mjini kupitia CCM alitetea serikali ya chama chake na jinsi kinavyoshughulikia sekta hizo katika mdahalo huo uliorushwa moja kwa moja na kituo cha luninga cha Star Tv.

Mdahalo huo pia uliwashirikisha wawakilishi wengine na vyama vyao kwenye mabano ni Samson Mwigamba, (ACT Wazalendo), Rajab Hoza (UPDP),  Jacob Samwel (ADC) na Nderakindo Kessy (NCCR Mageuzi).

Dk Kigwangala alianza kupata wakati mgumu baada ya kuzungumzia mkakati wa CCM kuondoa tatizo la msongamano wa wagonjwa katika hospitali za serikali ambapo ilielezwa kuwa hali ilivyo sasa, kitanda kimoja kinalaza wagonjwa watatu huku kina mama wajawazito wakilala sakafuni.

Dk Kigwangala alianza kwa kupuuza madai hayo akisema kuwa ni kauli za kisiasa, hivyo kuwataka wananchi wazungumze mambo yenye uhalisia.

“Mimi nimekuwa daktari katika hospitali ya Muhimbili na baadaye Mwananyamala, sikumbuki ni mara ngapi nimewahi kuona wagonjwa watatu wakilala kitanda kimoja. Hizo ni siasa tu siyo tatizo kubwa,” alisema.

Hata hivyo, alifafanua kuwa serikali ya ijayo chini ya Dk John Pombe Magufuli itakuja na utaratibu wa kutoa matibabu bure kupitia mifuko ya bima ya afya.

Kauli hiyo ilipingwa na wawakilishi wengine katika mdahalo huo ambao kwa nyakati tofauti walisema  kauli ya Dk Kigwangala inawakilisha mtazamo wa chama dola ambacho hakijali wananchi wake.

“Mimi sijawahi tu kuona wagongwa watatu wakilala kitanda kimoja, nimewahi pia kuona wagonjwa wakilala chini. Mama yangu alipokuwa akijifungua mtoto wa sita alijifungulia kichakani,” alisema Mwigamba ambaye alieleza kuwa ACT-Wazalendo itakuja na sera ya kuongeza bajeti ya afya kukabiliana na hali hiyo.

Kwa upande wake, Kessy alimshanga Dk Kigwangala akieleza kuwa hii ni dalili ya chama hicho kutowajali wanananchi.

Hoja nyingine iliyompa wakati mgumu Dk Kigwangala ni swali lililotaka aeleze kama kuna uhalali wa walimu kuwachapa wanafunzi kwa sababu ya wazazi wao kushindwa kutoa michango na kama ni halali kwa baadhi ya walimu kutoa mafunzo ya ziada.

Akijibu swali hilo, Dk Kigwangala alitaka jamii kutowadharau walimu akisema kuwa wanafanya kazi nzuri na ndiyo maana wameongeza ufaulu wa wanafunzi.

“Napenda tuwaheshimu na kuwatia moyo walimu badala ya kuwakatisha tamaa. Siyo vibaya walimu kuwa wajasiriamali katika maeneo ya kazi,” alisema Kigwangala.

Wakati daktari huyo wa magonjwa ya binadamu akieleza kuwa kila Mtanzania ana haki sawa ya kutibiwa nje ya nchi, wawakilishi wengine walidai fursa hiyo inatolewa kwa viongozi wa serikali ya CCM pekee.

“Hizi ni chuki za kisiasa ambazo watu wanaeneza kuwa ni viongozi pekee ndio wanaotibiwa nje. Ukweli ni kwamba, ili mtu akatibiwe nje, lazima madaktari watatu wathibitishe na hili linafanyika kwa Watanzania wote,”alisema Dk Kigwangala.