Rais Kikwete Amtaja Mhusika wa Sakata la Richmond....Asema ni Yule Anayetembea na Tundu Lissu Kila Siku Kwenye Kampeni - MULO ENTERTAINER

Latest

16 Sept 2015

Rais Kikwete Amtaja Mhusika wa Sakata la Richmond....Asema ni Yule Anayetembea na Tundu Lissu Kila Siku Kwenye Kampeni

Rais Jakaya Kikwete amesema anashangazwa na Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu kumtaka amtaje mhusika wa Richmond wakati mwenye Richmond yupo na anatembea naye mikoani.

Kikwete aliyasema hayo jana wakati akiwaaga wananchi wa Kigoma katika Uwanja wa Lake Tanganyika na kumtaka Lissu amtaje mwenye Richmond.

“Endapo Tundu Lissu atashindwa kumtaja mwenye Richmond, nitatoka hadharani na kumtaja mwenyewe,” alisema Kikwete.

Kabla ya mkutano huo, Rais Kikwete alifungua jengo la Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii, (NSSF) ambalo limejengwa kwa Sh7 bilioni.

Akifungua jengo hilo, aliwaomba wawekezaji na mifuko ya kijamii kuiga mfano wa NSSF kwa kuwekeza katika sekta ya majengo kwa kuwa yanapendezesha mji.

Kadhalika, Rais Kikwete alizindua jengo la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na nyumba 36 za bei nafuu zilizopo katika eneo la Mlole, Kigoma Mjini.

Suala la Richmond imekuwa moja ya ajenda za CCM katika kampeni za urais hasa baada ya Waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa aliyejiuzulu wadhifa huyo kwa kashfa hiyo kuhamia upinzani.

Kila sehemu ambako mgombea urais wa CCM anakwenda, suala hilo limekuwa likiibuliwa, huku Lowassa akisema yeye hakuhusika, bali alijiuzulu kuiokoa Serikali isianguke kwa kuwa ulikuwa uamuzi wa wakubwa.

Mgombea urais wa CCM, Dk John Magufuli amekuwa akienda mbali zaidi akisema akichaguliwa ataanzisha mahakama maalumu ya kushughulikia mafisadi wanaosababisha umaskini nchini.