Vurugu ndani ya UKAWA zasambaa mikoa 4 - Mtwara, Tabora, Kilimanjaro na Morogoro... - MULO ENTERTAINER

Latest

19 Sept 2015

Vurugu ndani ya UKAWA zasambaa mikoa 4 - Mtwara, Tabora, Kilimanjaro na Morogoro...

VURUGU zinazoendelea ndani ya umoja wa vyama vinne vya upinzani (Ukawa), kuhusu kuachiana majimbo na kata baada ya kusambaa katika mikoa ya Mtwara, Tabora na Kilimanjaro, sasa zimegonga hodi mkoani Morogoro.

Hali hiyo ambayo imevuruga hadi majimbo ya wenyeviti wenza wa Ukawa, ni tofauti na mtafaruku mwingine unaoendelea ndani ya chama kimoja katika safu za uongozi wa juu, ambazo zimepewa jina la ‘kushuka njiani wakati safari ikiendelea’.

Mkoa wa Morogoro una majimbo 11 ya uchaguzi, ambapo CUF katika mgawo huo ilipewa majimbo mawili ambayo ni Kilosa na Morogoro Kusini Mashariki na Chadema ikanyakua majimbo tisa.

Morogoro

Akizungumza na gazeti hili mjini Morogoro jana, mgombea wa Ubunge wa Jimbo la Kilosa, Abeid Mlapakolo (CUF), alisema pamoja na kuwa na makubaliano hayo, ameshangazwa kuona Chadema imemsimamisha mgombea ambaye anaendelea kufanya kampeni katika kata mbalimbali zilizomo kwenye jimbo hilo.

Kwa mujibu wa Mlapakolo, mgombea huyo wa ubunge wa Chadema, Rajab Msabaha, tayari ameshasambaza mabango na vipeperushi maeneo mbalimbali ndani ya jimbo hilo na amekuwa akifanya kampeni kinyume na makubaliano yaliyofikiwa na viongozi wa Ukawa.

Mlapakolo alidai mbali na kupiga kampeni, Msabaha pia alishiriki katika mapokezi ya mgombea wa urais wa Chadema anayeungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa alipowasili Kata ya Dumila iliyopo katika Jimbo la Kilosa Septemba 15, mwaka huu na wafuasi wake kadhaa.

“Jimboni ni vurugu tupu, wafuasi wa Chadema wananivurugia shughuli za kampeni...mimi ndiye mgombea halali wa Ukawa Jimbo la Kilosa, lakini ndugu zangu hawa wamemweka mgombea wao wa ubunge,” alisema na kuongeza.

Vurugu hizo zimemkuta pia mgombea wa ubunge wa Jimbo la Morogoro Kusini Mashariki, Salama Omary (CUF) ambaye amesema licha ya jimbo hilo kupewa CUF, Chadema nao wamemsimamisha mgombea wa ubunge kinyume na makubaliano.

Salama alisema bado mgombea wa ubunge wa Chadema, David Lugakingira, anaendelea kufanya kampeni za uchaguzi licha ya viongozi wake kumtaka asifanye hiyo.

Hatua

Kutokana na hali hiyo, Mlapakolo na Salama wameamua kuwasilisha malalamiko kuhusu Chadema kukiuka makubaliano hayo kwa mgombea wa urais wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania kupitia Chadema, Edward Lowassa, anayeungwa mkono na Ukawa.

Mlapakolo amesema tayari amefikisha suala hilo mbali na litashughulikiwa na viongozi wa Taifa wa Ukawa, ambao wanatarajiwa kwa kupeleka timu ya viongozi kwenda kutatua sakata hilo.

Naye Salama amefikisha sakata hilo kwa Lowassa ambaye alidai kuwa mgombea urais huyo aliahidi kufanyia kazi malalamiko hayo na kufikia uamuzi wa pamoja wa viongozi wa Ukawa.

Mtwara, Makaidi Mkoani Mtwara tangu mwanzoni mwa mwezi huu, mgombea ubunge wa Jimbo la Masasi ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, Dk Emmanuel Makaidi (NLD), alijikuta akikataliwa na wananchi katika vijiji mbalimbali vya jimbo hilo kila anapopanda jukwaani, huku wengine wakimzomea wakidai kuwa yeye sio chagua lao.

Dk Makaidi mwenyewe alipoulizwa alikaririwa akisema hawezi kukatishwa tamaa na kikundi cha watu wachache, kinachopiga propaganda zisizo na msingi, huku akiwataka wakazi wa Masasi, kuamini kuwa uteuzi wa majimbo uliofanywa na Ukawa, umezingatia misingi ya makubaliano ya umoja huo.

Akijaribu kuweka mambo sawa, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mtwara, Kassimu Bingwe, alikaririwa akisema mgawanyo wa majimbo uliofanywa na uongozi wa Ukawa Taifa, ulitoa ridhaa kwa NLD kuweka wagombea Masasi, Ndanda na Lulindi na kudai kuwa kinachotokea ni njama za wapinzani.

Hali hiyo ya Masasi, ilisababisha Mgombea Mwenza wa Ukawa, Juma Duni Haji, alipotembelea jimbo hilo kushindwa kuhutubia baada ya wafuasi wa CUF, kupiga kelele za kumkataa Makaidi, huku wakisisitiza kumtaka Ismail Issa Makombe maarufu Kundambanda, ambaye alikuwa mgombea wa CUF kabla ya kuondolewa na Ukawa.

*Kilimanjaro, Mbatia

Katika Mkoa wa Kilimanjaro kwenye Jimbo la Vunjo, wagombea udiwani 16 kutoka Chadema, juzi walitangaza kutomuunga mkono mgombea ubunge wa Vunjo kupitia NCCR-Mageuzi, ambaye pia ni Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia.

Mmoja wa madiwani hao, ambaye ni mgombea wa kata ya Mamba Kusini, Fredy Shayo, alisema hali hiyo imetokea baada ya vyama hivyo kushindwa kuelewana katika makubaliano ya kusimamisha mgombea mmoja, ambapo Chadema na NCCR-Mageuzi vimesimamisha wagombea wao wa udiwani kwenye kata zote 16 za jimbo la Vunjo.

Katibu wa Chadema Jimbo la Vunjo, Emmanuel Mlacky alikiri kuwa mwenendo wa Ukawa katika jimbo hilo haupo vizuri, kwa sababu unahatarisha uhai wa Chadema pamoja na uhai wa Ukawa.

Mlacky alisema maridhiano ya Ukawa yalilenga kumsimamisha mgombea mmoja kuanzia ngazi ya urais, wabunge na madiwani ambapo baada ya makubaliano hayo jina Mbatia liliridhiwa na viongozi wakuu wa umoja wao, huku ngazi ya madiwani ikiachiwa mamlaka ya jimbo kuona namna ya kusimamisha wagombea wa udiwani.

Alisema licha ya kukaa kwenye vikao vya maridhiano zaidi ya mara nane bila mafanikio, lakini viongozi wa NCCR wameona baada ya Mbatia kupitishwa na Makao Makuu kwa makubaliano, wamefikiri ndio inawapa nafasi ya kusimamisha madiwani karibia kata zote, jambo ambalo ni kinyume.

Katibu wa Chadema mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema, alisema haungi mkono madiwani wa chama chake kumsusia Mbatia, pia chama chake hakiungi mkono kubaguliwa kwa wagombea udiwani wa Chadema na mgombea huyo wa ubunge.

Naye Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya NCCR-Mageuzi, Heme Msabaha alisema, mambo yanayoendelea yanawapa ishara kuwa huenda Chadema wakawa wanatumika kwa lengo baya.

Simiyu, Regina

Katika Mkoa wa Simiyu, uzinduzi wa kampeni za mgombea ubunge wa Jimbo la Itilima kupitia Chadema, Martine Magire, uliingia doa baada ya wafuasi wa CUF wakiongozwa na mgombea ubunge wa chama hicho katika jimbo hilo, Martine Makondo, kuvamia na kufanya vurugu katika uzinduzi huo.

Kutokana na vurugu hizo, mke wa mgombea urais wa Chadema, Lowassa ambaye alikuwa mgeni rasmi, Regina Lowassa, aliondolewa jukwaani dakika 15 baada ya kuwasili katika uzinduzi huo.

Chanzo cha vurugu hiyo, ni mgombea huyo wa CUF aliyeingia katika uzinduzi huo akiwa amebebwa na wafuasi wake, kudai kuwa amehujumiwa na mgombea wa Chadema na kusababisha jina lake likatwe na Kamati Kuu ya chama chake.

Kamanda wa Polisi wa Simiyu, Gemin Mushy, alikaririwa akisema askari walitumia busara na kuepuka kumtoa mgombea huyo wa CUF jukwaani, kwa kuwa mazingira hayakuruhusu kumkamata.

Bundi NCCR

Wakati hali ikiwa hivyo majimboni na katika kata, migogoro katika safu za uongozi za vyama hivyo vinavyounda Ukawa, baada ya kutoka Chadema na CUF, sasa imehamia NCCR-Mageuzi.

Tayari aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa, ameshaachana na chama hicho katika migogoro hiyo, huku aliyekuwa Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, akijiuzulu nafasi zote ndani ya chama chake na kubakia mwanachama wa kawaida.

Lakini juzi, Makamu Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Leticia Mossore akiwa na Katibu Mkuu wa NCCR, Mosena Nyambabe na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Kamati Kuu, walimua kupingana na Mwenyekiti wao wa Taifa, Mbatia, mbele ya waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam.

Katika mkutano wao na waandishi wa habari, Mossore alilalamika kuwa Ukawa imekuwa ikimshirikisha Mbatia peke yake kutoka NCCR-Mageuzi na kuacha wengine, huku wanachama waliohama CCM, wakipewa umuhimu mkubwa kuliko walioasisi umoja huo.

Makamu Mwenyekiti huyo alisema kinachoonekana ni CUF kuwa Ukawa-Zanzibar, kwa kuwa haijali yanayoendelea Tanzania Bara na Chadema imekuwa ndiyo Ukawa-Tanzania Bara, kwa kuwa haijali yanayoendelea Tanzania Bara, huku NCCR-Mageuzi ikijikuta haipo popote, badala yake ikidhoofika siku hadi siku.

Mossore alifafanua katika taarifa yake kwa waandishi wa habari, jinsi Ukawa ilivyoshindwa kupata muafaka wa kuachiana majimbo.

“Kwa mfano, NCCR-Mageuzi tuliachiwa majimbo 12 tu ya Kasulu Vijijini, Kigoma Kusini, Muhambwe, Kasulu Mjini, Vunjo, Ileje, Mbinga Mjini, Manyovu, Buyungu, Ngara, Nkenge na Korogwe Mjini. Ikumbukwe kwamba mwaka 2010, NCCR-Mageuzi ilisimamisha wagombea katika majimbo 67. Kwa maana hiyo UKAWA umeturudisha nyuma katika kupata wabunge na kuimarisha chama zaidi ya miaka 20 baada ya kuundwa kwake,” ilifafanua taarifa yake hiyo kwa waandishi, aliyoitoa pamoja na Nyambabe.

Taarifa ilisema, “Licha ya kukubaliana kwamba NCCR-Mageuzi iachiwe majimbo 12, wenzetu wa vyama vingine katika UKAWA wamesimamisha wagombea katika majimbo 6 kati ya hayo. Wametuvunja moyo na kutuonesha kwamba hawatujali. Tuna mifano mingi ya kuonesha jinsi wagombea wetu wanavyofanyiwa vurugu. Pia tumeshindwa kupata muafaka wa namna ya kuachiana wagombea udiwani katika kata nyingi”.

Mossore na Nyambabe walimshauri mwenyekiti wao, Mbatia, aitishe vikao vya kikatiba ili waweze kujadiliana kuhusu hatima ya NCCR. Pia, walimshauri Mbatia asiwe msemaji wa Chadema wakati anakiacha chama chake cha NCCR kinadhoofika.

“Kwa mfano, Dk Slaa alipoishambulia Chadema hakuna kiongozi wa Chadema aliyemjibu, isipokuwa Mbatia ndiye aliyeamua kujiingiza kwenye ugomvi ndani ya Chadema.” Ilisema taarifa hiyo. Taarifa ilisema, “Tutachangishana ili tusafiri kwenye majimbo na kata za wagombea wetu na kuwasaidia kwenye kampeni ili wasibaki wapweke kama yatima”.

Taarifa hiyo ya NCCR ilisema, “Tunasisitiza kwamba upinzani wa kweli nchini hauwezi kujengwa kwa njia za hila, kwa kukiuka taratibu za kidemokrasia tulizojiwekea wenyewe, kwa kukiuka misingi muhimu kama uadilifu, kwa kuweka mbele tamaa na maslahi binafsi kuliko taifa, kwa kutegemea propaganda”.

Imeandikwa na John Nditi, Morogoro na Arnold Swai, Vunjo.