Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro ameongeza adhabu ya faini kutoka Tsh. milioni 3 hadi milioni 5 kwa Msanii Seif Kisauji (Babu wa TikTok) akimtaka Msanii huyo aombe msamaha hadharani kutokana na kosa la kurusha maudhui ya sanaa yanayokiuka maadili mtandaoni.
Waziri Ndumbaro ametoa uamuzi huo leo September 03, 2024 Jijini Dodoma baada ya kusikiliza rufaa ya Msanii huyo ya kupinga adhabu aliyopewa na Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ya kufungiwa kujihusisha na shughuli za sanaa kwa miezi 6 pamoja na kulipa faini ya shilingi milioni 3 kutokana na kurusha mtandaoni picha za video zinazokiuka maadili.
Kufuatia rufaa hiyo, Kisauji amekiri kosa la kusambaza maudhui hayo na kuomba apunguziwe adhabu hatua iliyomfanya Waziri Dkt. Damas Ndumbaro amuondolee adhabu ya kifungo cha cha miezi 6 cha kutojihusisha na shughuli za sanaa huku akimuongezea kiwango cha faini kutoka milioni 3 hadi 5.
“Sheria ya BASATA iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2019 kifungu cha 15 A inampa mamlaka Mhe. Waziri kusikiliza rufaa na kutoa maamuzi, hivyo kwa kushauriana na Naibu Waziri Hamis Mwinjuma ambaye ndiye Msimamizi wa Sekta ya Sanaa, nimefuta adhabu ya miezi sita aliyopewa kuanzia leo, na ninamtaka azingatie maadili katika kufanya kazi zake”
Awali katika kikao hicho Naibu Waziri Mwinjuma amemtaka Msanii huyo, kurudi katika sanaa aliyokua akiifanya zamani ambayo ndiyo iliyomfanya jamii imtambue na kuelewa kuwa yeye ni kioo cha jamii hivyo anapaswa kufanya Sanaa inayoelimisha na kuburushisha jamii bila kuharibu mila na desturi za Kitanzania