MKUU wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda kwa kushirikiana na kampuni ya Push Mobile leo wamezindua mfumo mpya wa utoaji taarifa ya uzembe unaofanyika katika sekta muhimu zilizopo wilayani humo.
Huduma hiyo itawahusu wananchi waishio Wilaya ya Kinondoni tu. Wananchi hao watapata fursa ya kutuma ujumbe kwa njia ya simu ya mkononi ambao utamfikia Makonda moja kwa moja na hivyo kumwezesha kushughulikia kero husika.
Akizungumza na waandishi wa habari leo ofisini kwake Jijini Dar es Salaam, Makonda amesema, wananchi wanatakiwa kutoa taarifa kuhusu kero za huduma muhimu kuanzia tiba mahospitalini, usafiri barabarani, mahakamani, masuala ya ardhi, polisi na maeneo ya biashara.
“Kwa mfano mtu uko eneo la biashara au uko katika kituo cha polisi umekaa kwa muda mrefu hakuna huduma, ukiuliza unajibiwa vibaya, au upo mahakamani kesi yako inazungushwa kwa muda mrefu mahakimu hawapo. Kuanzia hapo hapo ulipo unaweza kutuma malalamiko yako kwa kuandika neno ‘Kinondoni’ kisha unaacha nafasi, halafu unaandika kero yako kwa kifupi kwenda namba 15404. Ujumbe huo utanifikia moja kwa moja nami nitachukua hatua stahiki,” amesema Makonda.
“Nimewaandaa vijana wangu wasiopungua watano ambao nitafanya nao kazi watakuwa wakipokea ujumbe kutoka kwa wananchi na kuweza kutambua kama ni ukweli au uongo. Tutamtambua mtu huyo aliyetuma ujumbe eneo alipo kwa kutumia kompyuta zilizounganishwa kwenye mitambo maalumu na kisha tutafuatilia”. Amesema Makonda.
Makonda alisema kwamba, mkakati huo utakuwa ni endelevu ambapo wananchi wa Kinondoni watatuma ujumbe kwa masaa 24. Mkakati huu umepewa jina la “Sukuma twende”.
“Kila wiki nitakuwa nakutana nafanya tathmini ili kuangalia ni sekta ipi imelalamikiwa sana. Ikionekana ipo iliyobeba kero nyingi nitawaandikia barua za onyo, au kuagiza watumishi wabadilishwe vitengo kwa kupelekwa hata kijijini, kama sio kuwafukuza,” amesema Makonda.
13 Nov 2015
New
Makonda Afuata Nyayo za Dk John Magufuli Azindua ‘Sukuma Twende’ Kinondoni Kuwakomesha Watendaji Wabovu wa Serekali
mulo
Siasa