Watoto wawili wa Darasa moja wafariki kwa kujinyonga - MULO ENTERTAINER

Latest

23 Feb 2019

Watoto wawili wa Darasa moja wafariki kwa kujinyonga


Wanafunzi wawili wa Darasa la tano Shule ya Msingi Mikiroy Magugu Mkoani Manyara waliokuwa wanakaa Dawati moja wamefariki dunia katika matukio yanayofanana, wa kwanza alifariki Mwezi Januari mwaka huu kwa kujinyonga, mwingine amejinyonga februari 20.

Mwanafunzi huyo (11) wa darasa la tano Shule ya Msingi Mikiroy kijiji cha Magugu kata ya Magugu Wilaya ya Babati Mkoani Manyara amejinyonga kwa taulo hadi kufa.

Akizungumza na MUUNGWANA BLOG Mtendaji wa Kijiji cha Magugu Leonsi Daniel Lumbu  ameeleza kuwa  tukio hilo limetokea Februari 20 mwaka huu baada ya mwanafunzi huyo kutoka Shuleni majira ya Jioni ambapo hakuwakuta wazazi wake ndipo alipoenda kwa jirani kuchukua ufunguo na kuingia ndani na kujinyonga kwa taulo hadi kufa.

Amesema ni mtoto ambaye anaishi na Mama yake ambaye ameolewa na mwanaume mwingine huku baba yake mzazi akimuacha tangu alipokuwa na miaka miwili baada ya kufarakana.

Mtendaji huyo amemtaja Mwanafunzi huyo kuwa ni Mathayo Ezekiel huku akieleza kwamba Sio tukio la kwanza kutokea kwani January mwaka huu 2019 mwenzake waliokuwa wanasoma darasa moja na kukaa katika Dawati moja naye alikufa kwa kujinyonga hali iliyowaacha wengi midomo wazi wakijiuliza kulikoni?

Amewataka Wazazi kuwa waangalifu na Watoto muda wote waangalie mara kwa mara mienendo yao na kuwa na muda wa kuzungumza nao ili kujua matatizo yanayowasumbua.

Hata hivyo kumeibuka mzozo wa kugombea maiti kati ya baba mlezi na baba mzazi yupi anastahili kuuzika mwili huo, hali iliyopelekea Uongozi wa Kijiji kuingilia kati na kushauri waende Mahakamani na kusikiliza amri itakayotolewa na Mahakama.