Kwa mara ya kwanza tangu Kamati Kuu ya CCM ilipomuengua kwenye kinyang’anyiro cha uspika, Samuel Sita ambaye alikuwa Spika wa Bunge la Tisa, jana ameweka bayana mustakabali wake; ameamua kustaafu siasa.
Sitta aliongoza kwa mafanikio Bunge la Tisa kiasi cha kumfanya apewe kirahisi uenyekiti wa Bunge la Katiba na hivyo kujijengea jina miongoni mwa wana-CCM kiasi cha kujitumbukiza kwenye mbio za urais na baadaye kutaka kurudi tena kuliongoza Bunge la Kumi na Moja.
Lakini hakufanikiwa kupitishwa kuwania urais wala kugombea uspika, ambao aliahidi kuwa angeengulkiwa angefika hata mahakamani.
Lakini jana alikuwa na kauli tofauti.
“Mambo ya siasa kwa sasa basi,” alisema Sitta alipoulizwa na kuhusu mipango yake ya baadaye baada ya kutopitishwa na CCM kuwania uspika.
Sitta ambaye amewahi kuongoza wizara mbalimbali, alisema kwa sasa anajikita katika uandishi wa vitabu na kwamba kwa umri alionao na utumishi wake serikalini, umefika wakati kwake kupumzika na kutoa ushauri wa masuala mbalimbali kwa wale watakaohitaji mchango wake.
Novemba 15, Kamati Kuu ya CCM ilimtosa Sitta na wengine waliojitokeza kuwania uspika na badala yake ikateua majina matatu kwa ajili ya kupigiwa kura na wabunge wa CCM, ambao walimchagua mbunge wa Kongwa, Job Ndugai kuwa Spika.
Kuenguliwa kwa Sitta kulikuwa ni pigo lake la pili katika nafasi ya hiyo baada ya kukatwa na kikao hicho mwaka 2010 alipokuwa akitetea nafasi yake. Wakati huo Anne Makinda alichaguliwa kuongoza Bunge la Kumi lililomaliza muda wake mwaka huu.
Sitta alijizolea sifa wakati akiwa Spika wa Bunge la Tisa kuanzia mwaka 2005 hadi 2010, baada ya kuliongoza kuibua mijadala mbalimbali dhidi ya Serikali na kashfa ya Richmond iliyomfanya Edward Lowasa kujiuzulu uwaziri mkuu.
Baada ya kung’atuka
Alipoulizwa atajishughulisha na nini baada ya kustaafu, Sitta ambaye pia alikuwa mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba alisema: “Nipo tu nyumbani nimepumzika. Naridhika na niliyoyafanya kwa Taifa. Wale watakaotaka kupata ushauri wakinifuata nitawasikiliza.”
Alisema kwa sasa anaandika makala ambazo baadaye ataziweka katika kitabu chake kitakachoeleza hali ya nchi na historia za masuala mbalimbali.
“Ninachokiandika ni mtazamo wangu binafsi, ni jinsi ambavyo mimi ninaona kwa macho yangu,” alisema.
Alipoulizwa kama atakubali kuongoza wizara iwapo Rais John Magufuli atamteua kuwa mbunge na kisha waziri alisema: “Tusizungumze jambo ambalo halina mwelekeo huo.”
Hata hivyo, alisema kwa mtazamo wake hadhani kama anaweza kufikiriwa kuwamo katika baraza hilo.
Kupinga uspika kortini
Kuhusu sakata la uspika, Sitta alisema angekwenda mahakamani kupinga kuondolewa kwake, kama tu mchakato wa chama hicho ungefanyika bila kufuata taratibu na watu kuonewa.
Katika mazungumzo yake na Radio Uhuru FM wakati wa mchakato wa uspika, Sitta alisema kutokana na hali ya joto la kisiasa ilivyo, ambayo ilidhihirika zaidi wakati wa uchaguzi, wabunge walioshinda ni vijana na ni wazi spika anayehitajika ni mwenye uzoefu.
Alisema licha ya kwamba wapo waliojaribu kumshawishi asigombee nafasi hiyo tena, badala yake awe anatoa ushauri pale inapobidi, alisisitiza bado ana wito wa kuwatumikia wananchi kwa njia hiyo.
“Niliposema (nitakwenda mahakamani) kama nisipoteuliwa na CCM kuwania uspika nililenga kama kitatokea kitu kama uonevu. Yaani kama vingeletwa vigezo ambavyo havipo katika mchakato,” alisema.
“Kama unakumbuka mwaka 2010 kililetwa kigezo cha ‘spika mwanamke’. Hicho ndicho kitu ambacho nilikilenga kwamba kikijitokeza sitakikubali. Uzuri ni kuwa hakikuwapo na kumbuka kuwa jambo lile (la kupitishwa kuwania uspika) lilikuwa ni uamuzi wa chama si mtu,” alisema Sitta.