CHADEMA Yaionya CCM Umeya Dar es Salaam - MULO ENTERTAINER

Latest

20 Dec 2015

CHADEMA Yaionya CCM Umeya Dar es Salaam

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimemteua diwani wa Ubungo, Isaya Charles kugombea nafasi ya Meya wa jiji la Dar es Salaam, na kuitahadharisha CCM hakitakubali kuchezewa rafu katika uchaguzi huo.

Aidha, Chadema imemtangaza diwani wa Ubungo, Boniface Jakob kuwa mgombea wa nafasi ya Meya wa Kinondoni na diwani wa kata ya Bonyokwa, Charles Kuyeko kugombea umeya wa Ilala.

Uteuzi huo ulitangazwa jana jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu Chadema (Zanzibar), Salim Mwalimu wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.

Majina hayo yaliteuliwa kwa ushirikiano ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), alisema.

Mwalimu alisema wanatarajia kuona uchaguzi huo ukifanyika kwa amani na utulivu bila kuwepo na ubadilishwaji wa matokeo, kwa kuwa kuna mbinu chafu zinazofanywa na CCM sasa.

Alisema katika Halmashauri za Ilala na Kinondoni Chadema inaongoza kuwa na madiwani wengi lakini cha kushangaza CCM imekuwa haitaki kuyakubali matokeo hayo na kutaka kuyabadilisha.

"Kwa mujibu wa taratibu zilivyo ni kwamba Hamashauri yenye madiwani wengi ni kuwa chama hicho huchukua ushindi lakini hawa wenzetu CCM wamekuwa hawataki," alisema.

"Mfano mzuri katika Wilaya ya Temeke madiwani ni wengi wa CCM tumekubali huo ushindi kwa kuwa ni kweli wametuzidi.

"Kinondoni na Ilala hawataki umeya uchukuliwe na Chadema licha ya kuwa na madiwani wengi na sisi hatuwezi kukubali njama za wazi zinazofanywa na CCM.
"Na hata meya wa jiji lazima atoke Chadema kwa kuwa katika mkoa wa Dar es Salaam tunaongoza kuwa na madiwani wengi."

Mwalimu alisema ameshangazwa na kitendo cha CCM kwenda Zanzibar kuchukua wabunge kwa ajili ya kupigia kura Kinondoni.

Alisema kitendo cha wabunge hao kukubali jambo hilo ambalo ni la aibu katika jamii inayowazunguka ni sawa na kuwazalilisha Wazanzibari kuwa hawajasoma.

"Unakubalije kubebwa kutoka Zanzibar kuja kupigia kura meya wa Kinondoni! Hivi kabisa mwenyekiti wa chama cha CCM anakubali hii aibu ya wazi wazi isiyohitaji propaganda ya kuleta majeshi Zanzibar" "Hilo jambo tutalipinga kwa nguvu zote."

Pia Mwalimu ameitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) kuhakikisha inamaliza changamoto zote zilizojitokeza katika viti maalum vya udiwani.

"Huko Kelwa tumeshinda viti vya udiwani 13 na CCM wameshinda 11 katika mgawanyo wa viti maalum Chadema wamepatiwa viti vinne na CCM imepatiwa vitano,? alisema.

"Hapa tumeitaka NEC itueleze huo mgawanyo umegawanywa vipi" Tumeenda kuwauliza wanatueleza Mkurugenzi hawampati kwenye simu ili athibitishe ni nani mwenye madiwani wengi. Eti mkurugenzi hapatikani na mwezi umeshapita."