Haya Hapa Ndio Majipu Yaliyotumbuliwa Kwa Mpiga na Mawaziri wa Rais John Pombe Magufuli - MULO ENTERTAINER

Latest

24 Dec 2015

Haya Hapa Ndio Majipu Yaliyotumbuliwa Kwa Mpiga na Mawaziri wa Rais John Pombe Magufuli

MAWAZIRI wawili jana ‘walitumbua majipu’ baada ya kutangaza kusimamishwa kazi kwa Mtendaji Mkuu wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART), Asteria Mlambo na Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk Diwani Msemo, wote wakipisha uchunguzi dhidi yao.

Mlambo amesimamishwa kazi kuanzia jana ili kupisha uchunguzi baada ya serikali kubaini ukiukwaji wa wazi wa Sheria ya Manunuzi ya Umma katika kumpata mtoa huduma ya mpito wa mradi huo wenye nia ya kupunguza msongamano wa magari barabarani kwa madhumuni ya kurahisisha usafiri na usafirishaji jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, George Simbachawene alisema kutokana na kukamilika kwa sehemu ya ujenzi wa miundombinu ya Awamu ya Kwanza ya mradi, Serikali iliamua kuwa na mtoa huduma wa mpito kabla ya kumpata wa kudumu.

“Mtoa huduma wa mpito alipaswa kupatikana kwa mujibu wa Sheria ya Manunuzi ya Umma. Hata hivyo, Serikali imebaini ukiukwaji wa wazi wa sheria hiyo wakati wa kumpata mtoa huduma wa kipindi cha mpito.

Kufuatia hali hiyo nimeamua kumsimamisha kazi kuanzia leo tarehe 23 Desemba, 2015, Mtendaji Mkuu wa DART, Bi. Asteria Mlambo ili kupisha uchunguzi,” alieleza Simbachawene.

Simbachawene alizitaja sababu za kumsimamisha kazi Mtendaji Mkuu huyo wa DART kuwa ni kushindwa kuzingatia Sheria ya Manunuzi ya Umma wakati wa kumpata mtoa huduma katika kipindi cha mpito; kushindwa kuchukua hatua hata pale alipobaini kuwa mtoa huduma wa mpito amekiuka masharti ya mkataba wa kutoa huduma ya mpito; na kufanya maamuzi makubwa pasipo kuishirikisha Bodi ya Ushauri ya DART.

Aidha, alisema Serikali inatambua kuwa wapo watumishi wa DART ambao hawakumshauri vizuri Mtendaji Mkuu, hivyo watumishi hao watachunguzwa na kuchukuliwa hatua na Kaimu Mtendaji Mkuu atakayeteuliwa.

Nimemwagiza Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tamisemi kuendelea na taratibu za kinidhamu dhidi ya Mtendaji Mkuu aliyesimamishwa kazi,” alisema Simbachawene. Aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea kuchukua hatua kwa haraka na uangalifu ili mradi huu uanze kutoa huduma bora ya usafiri kwa wakazi wa Dar es Salaam bila kuchelewa zaidi, huku akiwaomba kuitunza na kuithamini miundombinu ya DART kwa kuwa imegharimu fedha nyingi kwa manufaa yao.

Wiki iliyopita, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alitembelea maeneo ya mradi huo wa DART na kuagiza kuwa uanze kazi Januari 10, mwakani baada ya kupigwa kalenda kwa muda sasa tangu mwaka jana.

Wakati Simbachawene akichukua hatua hiyo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amemsimamisha Dk Msemo kwa kile kilichoelezwa ni kupisha uchunguzi unaolenga kubaini iwapo mgongano wa kimaslahi umeathiri utendaji wa taasisi hiyo.

Aidha, watendaji wote wa serikali katika sekta ya afya hususan wakuu wa vituo vya kutolea huduma za afya, wafamasia, wauguzi na waganga wafawidhi, wameagizwa kukiri kwa maandishi ndani ya siku 21 kuanzia sasa endapo wanamiliki hospitali, zahanati, kliniki na maduka ya dawa.

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyosainiwa na Waziri Mwalimu, imefafanua uamuzi wa kumsimamisha Kaimu Mkurugenzi huyo wa Ocean Road, unatokana na ziara walizofanya kukagua utoaji wa huduma za afya katika maeneo mbalimbali ambako walibaini upungufu wa dawa umeendelea kujitokeza kwa wingi.

Baadhi ya wagonjwa walieleza kwa uchungu jinsi wanavyopata tabu ya kupata dawa hata zile ambazo wanatakiwa wazipate kwa bei ya ruzuku au zinazotakiwa kutolewa bure na serikali,” ilisema taarifa hiyo.

Kwa kuzingatia suala hili la mgongano wa kimaslahi, manung’uniko mengi kutoka kwa wapokea huduma, hususan katika Taasisi yetu ya Saratani ya Ocean Road, nimechukua hatua ya kumsimamisha kazi Kaimu Mkurugenzi,” iliongeza taarifa ya waziri huyo.