Spika wa Bunge Job Ndugai Yupo India kwa Matibabu. - MULO ENTERTAINER

Latest

17 Dec 2015

Spika wa Bunge Job Ndugai Yupo India kwa Matibabu.

Spika wa Bunge, Job Ndugai ni mgonjwa na yupo India kwa matibabu.

Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alisema jana kuwa Ndugai yuko nje ya nchi kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake bila ya kusema amekwenda nchi gani wala ugonjwa unaomsumbua.

Ni kweli Spika yupo nje, lakini alikwenda kwa ajili ya kufanya uchunguzi tu, siyo kwamba anaumwa sana, hapana ila hii ni mara ya pili kwenda kufanya uchunguzi huo. Hata ukitaka kuzungumza naye mpigie simu mtazungumza naye maana hali yake inaendelea vizuri na yuko salama,” alisema Dk Kashilila.

Balozi wa Tanzania nchini India, John Kijazi alipopigiwa simu ili kujua kama kiongozi huyo yuko huko, alisema:

Ni kweli yuko hapa India kwa matibabu na anaendelea vizuri. Unaweza kumpigia wewe mwenyewe uzungumze naye.” Alisema Kijazi bila kuweka wazi kwamba yuko hospitali gani na nini hasa kinachomsumbua.

Ndugai hajaonekana hadharani, kwa muda mrefu, hata katika shughuli muhimu za kitaifa ambazo zimekuwa zikifanywa na Rais John Magufuli, hivyo kuacha maswali mengi kutoka kwa wananchi.

Shughuli mojawapo ambayo Spika huyo hakuhudhuria ni ile ya kuapishwa mawaziri wapya Jumamosi iliyopita Ikulu, Dar es Salaam. Naibu Spika, Dk Tulia Akson ndiye alihudhuria.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI