Kiingereza Tatizo Darasa la Nne, Wanafunzi 109,000 Kurudia Darasa Baada ya Matokeo Kutoka - MULO ENTERTAINER

Latest

22 Jan 2016

Kiingereza Tatizo Darasa la Nne, Wanafunzi 109,000 Kurudia Darasa Baada ya Matokeo Kutoka

Jumla ya wanafunzi 108,829 sawa na asilimia 11.13 kati ya 977,886 waliofanya mtihani wa kitaifa wa darasa la nne mwaka jana, wanatakiwa kukariri darasa baada ya kupata ufaulu usioridhisha.

Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa jana na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania, Dk. Charles Msonde, somo lililofanya vibaya kwa kupata kiwango cha chini cha ufaulu ni Kiingereza.

Akitoa matokeo hayo jana, Dk. Msonde alisema kiwango cha ufaulu kwa somo la Kiingereza ni wa chini zaidi kwa asilimia 65.67 wakati Sayansi ufaulu wake ukiwa juu kwa asilimia 89.44.

Alisema jumla ya wanafunzi 1,037,305 waliosajiliwa kufanya upimaji huo kitaifa, wasichana walikuwa ni 535,273 sawa na asilimia 51.60 na wavulana walikuwa ni 502,032 sawa na asilimia 48.40.

Alisema wanafunzi 977,886 sawa na asilimia 94.27 ya waliosajiliwa, walifanya upimaji huo na kati yao wasichana walikuwa ni 510,211 sawa na asilimia 95.32 na wavulana walikuwa ni 467,675 sawa na asilimia 93.16.

Alisema wanafunzi 59,419 sawa na asilimia 5.73, hawakufanya upimaji huo ambapo wasichana ni 25,062 sawa na asilimia 4.68 na wavulana ni 34,357 sawa na asilimia 6.84.

UFAULU WA JUMLA
Dk. Msonde alisema jumla ya wanafunzi 869,057 kati ya 977,886, wamepata alama zenye daraja la ufaulu wa A, B,C na D.

Alisema wanafunzi 108,829 wamepata daraja la E lenye ufaulu  usioridhisha.

WANAFUNZI BORA KITAIFA
Aliwataja kuwa ni Frank Mgeta, kutoka Shule ya Msingi Twibhoki mkoani Mara, akifuatiwa na Salum Rashid, kutoka Shule ya Msingi Hazina, ya jijini Dar es Salaam.

Wengine na shule zao katika mabano ni Mussa Christian (Alliace Mwanza), Ezekiel Gilu (Waja Springs Geita), Martha Nkwimba (Tusiime, Dar es Salaam), Lameck Nsulwa na Rajabu Hamis (Rocken Hill, Shinganga), Charles Luhumbika (Kwema Shinyanga), Mathias Amos  na Idd Masoud ( Alliance Mwanza).

WASICHANA 10 WALIONG’ARA KITAIFA
Aliwataja na shule zao kwenye mabano kuwa ni Martha Nkwimba (Tusiime, Dar es Salaam), Sabina Athanas (Alliance English, Mwanza), Nervis Michael (Alliance English, Mwanza, Jenipher Nyachilo (Paradise English, Geita) na Vivian Lyimo (Imani Kilimanjaro).

Wengine ni Vaileth Emmanuel (Fort Ikoma, Mara), Beatrice Novatus (Kaizirege Kagera), Ayamu Ayoub (Kaizirege Kagera), Ashura Juma (Kaizirege Kagera) na Alinda Byamungu (St. Peter Claver Kagera).

WAVULANA 10 BORA KITAIFA
Dk. Msonde aliwataja kuwa ni Frank (Twibhoki Mara, Salim Rashid (Hazina Dar es Salaam), Mussa Christian (Alliance English Mwanza), Ezekliel Gilu (Waja Springs Geita) na  Lameck Nsulwa (Rocken Hill Shinyanga).

Wengine ni Rajabu Hamis ( Rocken Hill Shinyanga), Charles Ndaki (Kwema Shinyanga), Mathias Amos (Alliance English Mwanza), Idd Masoud (Alliance English Mwanza) na Godfrey Manazi (Alliance English Mwanza).

SHULE 10 BORA KITAIFA
Katibu huyo alisema iliyoongoza ni Shule ya Msingi Alliance ikifuatiwa na Waja Springs, St. Peter, Tumaini, Furaha, Acacia Land, Tusiime, Imani, Kaizirege na Evenezer.

MIKOA 10 ILIYOFANYA VIZURI
Aliitaja kuwa ni  Dar es Salaam ambayo imeongoza ikifuatiwa na Iringa, Kilimanjaro, Njombe, Arusha, Tanga, Geita, Kagera, Mwanza na Shinyanga.

Halmashauri 10 zilizofanya vizuri alizitaja kuwa ni Ilala, Moshi, Mji Njombe, Arusha, Mji Makambako, Tanga Mjini, Arusha, Mufindi, Hai na Bukoba Manispaa.

Dk. Msonde alitaka zifanyike juhudi za makusudi ili kuinua kiwango cha ufaulu kwa masomo ambayo wanafunzi wamefaulu kwa kiwango cha chini.

Alisema Baraza linafanya uchambuzi wa kina wa matokeo hayo kwa kila somo ili kubainisha mada mbalimbali zilizowatatiza wanafunzi na baadaye kutoa machapisho ya uchambuzi yatakayowasilishwa kwa wadau wa elimu.

Alisema lengo ni kuwawezesha walimu kutumia taarifa hizo katika kuboresha ufundishaji na ujifunzaji shuleni.

Dk. Msonde alisema baraza linawahimiza maofisa elimu wa mikoa na wilaya kufuatilia katika kuhakikisha kuwa ufundishaji na ujifunzaji wa maeneo yaliyohitaji mkazo unafanyika ipasavyo.