Seif Rais Zanzibar, Maandalizi ya Kutangazwa yaiva - MULO ENTERTAINER

Latest

2 Jan 2016

Seif Rais Zanzibar, Maandalizi ya Kutangazwa yaiva

USHINDI wa Maalim Seif Shariff Hamad katika uchaguzi mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, ungali salama.

MAWIO limeelezwa kuwa ushindi huo utadhihirishwa kabla ya Zanzibar kufikia kilele cha maadhimisho ya miaka 51 ya Mapinduzi.

Taarifa zinasema viongozi wa kitaifa, wakiwemo marais wastaafu Zanzibar, ambao wamekuwa wakikutana na Maalim Seif, Ikulu ya Zanzibar, wanakaribia kukamilisha utaratibu wa kuwezesha kiongozi huyo kutangazwa mshindi wa uchaguzi huo.
“Hili halina utata wowote. Nakuhakikishia wanakaribia kuona mantiki na kuelewana; utaratibu wa kumtangaza Maalim Seif utatolewa wakati muafaka,” amesema mwanadiplomasia kutoka moja ya mataifa ya Ulaya.

Amesema kwa kadri anavyofahamu, maendeleo ya mazungumzo hayo yanayomhusisha pia Rais Dk. Ali Mohamed Shein, katika siku za karibuni, yamejikita katika kupata uhakika kuwa serikali mpya itaundwa kwa kuzingatia matakwa ya sheria na katiba.

Lakini amesema, hata suala hilo halijawa tatizo kwa kuwa mfumo wa kuunda serikali umesukwa vema katika Katiba ya Zanzibar ya Mwaka 1984.

“Kama unavyojua mfumo wa serikali utakuwa uleule wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kwa matokeo ya uchaguzi vyama vya CCM na CUF ndivyo vitaunda serikali mpya,” alisema.
Mwanabalozi huyo aliulizwa na mwandishi jinsi anavyoona hali ya kisiasa kwa sasa na hasa kuhusu mgogoro uliotokana na uchaguzi.

Mgogoro wa sasa Zanzibar ulitokana na uchaguzi mkuu kufutwa kiubabe na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha.
Jecha alifuta uchaguzi kwa tangazo lililorushwa na Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) mchana wa Oktoba 28.

Wakati huo tayari Jecha alikuwa ameshatangaza kura za majimbo 33, akibakiza majimbo 21 tu.
Mwandishi alilenga kupata msimamo wa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu kauli tata za viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar.
Mwishoni mwa wiki iliyopita, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Zanzibar, Waride Bakari Jabu aliwataka wana-CCM kujiandaa kwa uchaguzi wa marudio aliosema utafanyika “wakati utakapowadia.”
Hata hivyo, kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari ndani ya CCM, Serikali ya Mapinduzi na Serikali ya Muungano, hakutakuwa na uchaguzi wowote bali utakuwepo utaratibu wa kumtangaza mshindi.
Chanzo katika CCM kimesema, “Hili liko wazi, mshindi wa uchaguzi ule ni Maalim Seif wa CUF ambaye naweza kusema amefanikiwa kusimamia ushindi wake huo na hoja zake hazishindiki. Nakwambia atatangazwa siku chache zijazo.”
Kiongozi huyo ambaye aliomba asitajwe jina gazetini, amemsifia Maalim Seif kwa kubaki mtulivu wakati wote akijadiliana na viongozi wenzake ambao wote ni kutoka CCM.

Katibu Mkuu huyo wa CUF na mwanasiasa ambaye amekuwa akilalamika kuhujumiwa mara zote akigombea urais, amekuwa akishiriki mazungumzo na marais wastaafu.
Marais hao ni Ali Hassan Mwinyi, Dk. Salmin Amour Juma, Amani Abeid Karume na Dk. Shein. Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi naye amehudhuria mazungumzo hayo.
Dalili za kuwepo muafaka katika majadiliano zimeonekana hivi karibuni pale Dk. Shein, aliyekuwa akigombea urais kwa mara ya pili, na Maalim Seif walipokutana na Rais mpya wa Tanzania, Dk. John Magufuli katika nyakati tofauti.

Wote walisikika wakisema majadiliano yao yanaendelea vizuri, lakini Dk. Magufuli akieleza waandishi wa habari nje ya ofisi yake Ikulu baada ya kukutana na Maalim Seif kuwa, “amenihakikishia wanaendelea vizuri na nimemtaka wakamalize majadiliano yao na apige kazi.”
Dk. Shein alipotoka nje ya maongezi na Dk. Magufuli aliwaambia waandishi wa habari kuwa mazungumzo yanaendelea vizuri na yatakapomalizika, watatoa taarifa kwa umma kuwaeleza maafikiano yaliyofikiwa.

Taarifa zilizopatikana baadaye zinasema moja ya mambo ambayo Dk. Shein alitakiwa kuyafanya baada ya hapo, ni kukutana na Kamati Maalum ya NEC-CCM, kuwaeleza maendeleo ya vikao na viongozi wenzake vinavyofanyika Ikulu.

Jumapili iliyopita, MAWIO lilielezwa kile kilichotokea katika kikao kilichofanyika Ofisi Kuu za CCM Kisiwandui mjini Zanzibar kilichoandaliwa kwa ajili ya Dk. Shein kutoa taarifa yake.
Katika kikao, Dk. Shein “alitoa taarifa yake na taarifa yenyewe kujadiliwa vizuri” mpaka kikao kilipomalizika yapata saa 9.30 alasiri.
Dk. Shein aliondoka na Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, mara baada ya kumaliza kikao.

Lakini baada ya viongozi hao wakuu kuondoka ukumbini, baadhi ya wajumbe waliobaki walianza kudai kuwa hawakubaliani na mapatano na kwamba wanataka uchaguzi urudiwe.
Gazeti hili limeambiwa baada ya Dk. Shein kuondoka Kisiwandui, Balozi Seif alifuatana na baadhi ya viongozi kwenda Ofisi ya Mkoa wa Mjini Magharibi, iliyoko Amani, ambako walifanya mjadala ulioibua kilichoitwa “kauli za chuki” zikimlenga Maalim Seif.

Kwa kuzingatia aliyoyasema Dk. Shein, baadhi ya viongozi walionekana wakifuta machozi kwa kilichoelezwa ni “kutoamini kwao kuwa CUF itapishwa kuongoza serikali mpya.”
Akijibu hoja ya kurudia uchaguzi ambayo wananchi wengi wameonesha kuipinga, Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Mawasiliano na Umma wa CUF, Ismail Jussa Ladhu amesema kurudia uchaguzi siyo chaguo la wananchi.

Aliwaambia waandishi wa habari mgogoro wa Zanzibar ni wa kutengeneza, uliolenga kuchanganya wananchi na kuwapora ushindi wao. Ametaka wananchi wapuuze kauli za kurudia uchaguzi.
“CUF inawahakikishia Wazanzibari kwamba haitotetereka; itasimamia kwa dhati maamuzi waliyoyafanya kwa njia za kidemokrasia kupitia uchaguzi mkuu na italinda chaguo lao la Rais wa Zanzibar, Wawakilishi na Madiwani wao,” alisema Jussa.

Amepongeza wananchi kwa kuonesha “ukomavu wa hali ya juu wa kisiasa na kuendelea kutunza amani na utulivu wakati wakisubiri matokeo ya kazi kubwa waliyoifanya tarehe 25 Oktoba ambayo inaashiria ujenzi wa Zanzibar Mpya.”

Ni msimamo wa CUF kuwa Maalim Seif alishinda uchaguzi kwa zaidi ya kura 25,000.
Kwamba CUF ilipata viti 27 vya uwakilishi. Kwamba CCM ilishindwa kupata kiti kisiwani Pemba. Kwamba CUF ilitwaa viti tisa Unguja.