Rais Magufuli ametoa maagizo hayo alipokuwa akizungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake njiani akiwa safarini kutoka Dar es salaam kwenda Dodoma ambapo amesema mkoa wa Morogoro ulikuwa na viwanda vingi na mashamba mengi makubwa ambayo kama waliouziwa wangeyaendeleza, yangezalisha ajira na kuongeza uzalishaji wa bidhaa za viwandani na Mazao ya kilimo, lakini waliouziwa mashamba na viwanda hivyo wameamua kutekeleza ama kubadilisha matumizi, huku baadhi wakitumia rasilimali hizo kuombea mikopo katika mabenki jambo ambalo serikali yake haitalikubali.
Rais Magufuli pia amesimamishwa na kuwasalimu wananchi wa Wami Dakawa, Magole na Dumila ambako pamoja na kuwahakikishia kuwa atatekeleza ahadi yake ya kuwapa mashamba atakayonyang’anya kutoka kwa walioyatelekeza, amewataka kuachana na migogoro kati ya wakulima na wafugaji badala yake watatue migogoro hiyo kwa kutumia njia za kisheria.
Aidha, amewataka viongozi wote wa Mkoa hadi vitongoji kushirikiana kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji kabla haijasababisha madhara, na ameonya kuwa migogoro hiyo ikileta madhara itakuwa ni kigezo tosha kwa viongozi hao wameshindwa kutekeleza wajibu wao na wanapaswa kuachia ngazi.