Upendeleo wa Ajira Watoto wa Vigogo: Mahakama Yawaachia Huru Watoto wa Vigogo BOT Waliokutwa na Vyeti Feki - MULO ENTERTAINER

Latest

4 Feb 2016

Upendeleo wa Ajira Watoto wa Vigogo: Mahakama Yawaachia Huru Watoto wa Vigogo BOT Waliokutwa na Vyeti Feki

Bank kuu ya Tanzania
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imewaachia huru watoto wanane wa vigogo waliokuwa wameshitakiwa wakidaiwa kupatiwa ajira katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kutumia vyeti vya kughushi, baada ya kutowakuta na hatia.

Walioachiwa huru ni Justina Mungai, Christina Ntemi, Siamini Kombakono, Janeth Mahenge, Beatha Massawe, Jacqueline Juma, Philimina Mtagurwa na Amina Mwinchumu.

Hakimu Mkazi Mkuu, Warialwande Lema, aliwaachia huru washitakiwa hao jana, alipokuwa akisoma hukumu ya kesi hiyo iliyochukua takribani miaka minane.

“Mahakama hii imewaona washitakiwa hawana hatia na kuwaachia huru kutokana na upande wa jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka dhidi yao pasi na kuacha shaka yoyote,” alisema.

Alisema wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, upande wa jamhuri ulileta mashahidi sita na vielelezo kadhaa na baada ya washitakiwa kuonekana wana kesi ya kujibu walijitetea wenyewe na kuleta vielelezo.

Alisema ni jukumu la upande wa jamhuri kuthibitisha mashitaka pasi na kuacha shaka yoyote na kwamba sio jukumu la mshitakiwa kuthibitisha kosa hilo.

Hakimu huyo alisema wakati wa usikilizwaji wa kesi hiyo, upande wa jamhuri uliwasilisha nakala za vyeti na kwamba ulishindwa kuwasilisha vyeti halisi kuonesha kipi halali na kipi cha kughushi.

Hakimu huyo alisema pia baada ya kufunga ushahidi pande zote ziliomba kuwasilisha hoja za kisheria iwapo zinaona washitakiwa wana hatia ama la, lakini hadi mahakama inatoa hukumu hakuna upande hata mmoja uliofanya hivyo.

Alisema upande wa jamhuri haukuleta shahidi aliyetengeneza vyeti hivyo badala yake walileta nakala tu za vyeti, hivyo upande wa jamhuri umeshindwa kuthibitisha mashitaka pasi na kuacha shaka yoyote.

Alisema upande wa jamhuri kama walikuwa na nia ya kuthibitisha kesi wangemleta mtaalamu wa maandishi ambaye angethibitisha iwapo vyeti hivyo vilikuwa vya kughushi ama la badala yake imebaki hisia tu.

Hakimu huyo alisema mahakama hiyo imesikiliza ushahidi wa kuhisi, kwa upande wa jamhuri kushindwa kuthibitisha mashitaka, hivyo imewaona washitakiwa hawana hatia na kuwaachia huru.

Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, washitakiwa hao walikuwa wakidaiwa kughushi vyeti vya kuhitimu kidato cha nne na kutoa hati za uongo kwa mwajiri wao ambaye ni BoT.