Nape Nhauye Atema Cheche..TFF Inao Uwezo wa Kumlipa Kocha Mkuu wa Taifa Boniface Mkwasa.. - MULO ENTERTAINER

Latest

31 Mar 2016

Nape Nhauye Atema Cheche..TFF Inao Uwezo wa Kumlipa Kocha Mkuu wa Taifa Boniface Mkwasa..

Serikali ya awamu ya tano kupitia Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye imesema kwamba Shirikisho la Mpira wa miguu nchini TFF linapaswa kumlipa mshahara kocha wa timu ya taifa (Taifa Stars,) kwa sababu uwezo wa kubeba majukumu hayo wanayo.

Charles Boniface Mkwasa alichukua nafasi ya M-holland, Marti Nooij, Juni 21 mwaka uliopita na ilisemwa kwamba serikali itaendelea kuisaidia TFF kumlipa kocha wa timu ya Taifa na Mkwasa (kocha wa kwanza mzawa tangu 2006) angeendelea kulipwa mshahara kama ule ambao makocha wa kigeni walikuwa wakilipwa.

Mbrazil, Marcio Maximo aliifundisha Stars kwa miaka minne kati ya 2006 hadi mwaka 2010, Mdenmark, Jan Borge Poulsen alichukua nafasi hadi mwaka 2012 tinu hiyo ilipochukuliwa na Mdenmark mwingine Kim Poulsen ambaye naye aliisimamia hadi mapema mwaka 2014 alipopewa majukumu hayo Nooij.

Makocha wote hao walikuwa wakilipwa mishahara yao na serikali iliyopita ya awamu ya nne chini ya rais mstaafu, Mh. Jakaya Mrisho Kikwete.

Licha ya TFF kusema kwamba Mkwasa ataendelea kulipwa kiasi cha Shililindi milioni 25 za kitanzania kama mshahara wake wa mwezi na serikali ya Kikwete kudai itaendelea kuwalipia, Mkwasa amelipwa mshahara huo mara moja tu (Mwezi Julai, 2015)

Kufikia mwezi huu katika mkataba wake imebainika kwamba kocha huyo anadai kiasi kisichopungua milioni 200 kama malimbikizo ya mishahara yake.

NI juzi tu rais wa serikali ya awamu ya tano, Mh. John Magufuli alisema kuwa serikali yake itapunguza kima cha juu cha mishahara na kufikia milioni 15 kama mshahara wa mfanyakazi, na kiwango cha chini alisema kitakuwa milioni 1.5 kwa maana hiyo mshahara wa Mkwasa (milioni 25 kwa mwezi) hautakiwi pia katika serikali yake.

Kitendo cha serikali ya awamu ya tano kusema kwamba, TFF inapaswa kumlipa mshahara kocha wa timu ya Taifa kinaweza kuonekana ni pigo kwa Mkwasa lakini kwa namna yoyote ile Shirikisho linapaswa kufanya hivyo kwa kuwa Stars ni timu yenye udhamini mkubwa, pia TFF wanaweza kutumia njia nyingie za kujiingizia kipato chao kupata pesa za kumlipa mshahara kocha wa Stars.

Kila mtu ameona kazi iliyofanywa na Mkwassa kuanzia mchezo wake wa kwanza dhidi ya Uganda katika harakati za kufuzu kwa fainali zilizopita za CHAN. Mkwassa amesema kwamba amekubali kufanya kazi yake bila tatizo licha ya kutolipwa mshahara kwa miezi 8.

Ndiyo kama alivyosema mwenyewe kwamba yeye ni ‘mzalendo’ ndiyo maana ameendelea kufanya kazi yake lakini umefika wakati wa TFF kuwajibika yenyewe tena kikamilifu katika malipo ya mishahara ya timu za Taifa.

Hakuna uzalendo wa kufanya kazi miezi nane mfululizo bila kulipwa mshahara na Mkwasa anaweza kuzungumza hivi kwa uoga tu ama kulinda kibarua chake lakini katika uhalisi ni kitendo ambacho hakifurahii. Naungana na Waziri aliyesema kwamba, TFF inapaswa kumlipa kocha wa timu ya Taifa kwa kuwa uwezo huo wanao.