Msipoteze Muda Wenu Kutarajia Bifu Kati ya Zitto na UKAWA Bungeni - MULO ENTERTAINER

Latest

1 Feb 2016

Msipoteze Muda Wenu Kutarajia Bifu Kati ya Zitto na UKAWA Bungeni

Zitto Kabwe
Madhumuni makuu ya chama chochote cha siasa ni kushika Dola. CCM imeshika Dola hivyo kazi kuu sasa ya chama cha upinzani ni kujiuza kwa wananchi ili ukifika mwaka 2020 kiweze kushika Dola.

Baada ya uchaguzi, platform kubwa kwa chama cha upinzani kwa ajili ya kujiuza ili kijiwekee mazingira ya kuwa na nafasi ya kushika Dola katika kipindi kijacho ni Bungeni na kazi pekee itakachokiwezesha chama cha upinzani kufanikiwa kwenye hili ni kuikosoa Serikali pamoja na kuiwajibisha pale ambapo inastahili kuwajibika.

Hivyo ni wazi kwamba vyama vyote vya upinzani vina mkakati mmoja nao ni kujenga hoja dhidi ya Serikali iliyoundwa na chama Dola ili kufikia malengo yake.

Hivyo ni wazi kwamba Bungeni ni mahali ambapo vyama vya upinzani havina jinsi bali kuunga mkono hoja zinazotolewa dhidi ya Serikali ama na wana CCM au wapinzani nje ya chama chao ambazo zina mashiko na kwa sababu hii si jambo la ajabu kwa vyama vya upinzani kulazimika kuungana mkono katika hoja zenye mashiko dhidi ya Serikali kama tunavyoshuhudia sasa hivi.

Ingawaje Zitto yuko peke yake kutoka chama cha upinzani cha ACT Wazalendo ukilinganisha na UKAWA ambao wako wengi kupitia tiketi za CHADEMA na CUF, bado Zitto ana kipaji kizuri tu cha kujenga hoja dhidi ya Serikali, hoja ambazo kila mpinzani lazima ataziunga mkono kama kweli anataka kufikia malengo yake ya kwenda Ikulu na kuepuka kudharauliwa na wapiga kura.

Vilevile Zitto itabidi aunge mkono hoja zinazowasilishwa na wapinzani wenzake ambazo zina tija katika kupaisha uhai na matarajio ya chama cha upinzani kuelekea Ikulu dhidi ya Serikali iliyowekwa madarakani na chama Dola kama kweli ana nia ya kukitayarisha chama chake kuwa na nafasi ya kushika Dola hapo 2020.

Hivyo tutarajie ushirikiano kati ya Zitto na UKAWA kuimarika bungeni kwa kipindi hiki cha miaka mitano na ninachokiona ni kwamba uchaguzi wa 2020 utakuwa na muungano wa wapinzani ambao unaweza kuwa na jina lingine badala ya UKAWA kama marekebisho yanayohitajika ya katiba yakifanyika kabla ya uchaguzi ujao lakini kwa vyovyote vile, iwe UKAWA ya sasa hivi au muungano mwingine bado ACT itakuwa chama ambacho kitakuwa na karata ya kuupa muungano wowote ule utakaobuniwa nguvu na matarajio makubwa ya kwenda Ikulu ifikapo 2020 kama Zitto ataendelea na kazi yake ya kuibana Serikali kama kawaida yake na kama Mwenyezi Mungu atampa busara ya kuendelea na harakati zake za kisiasa pamoja na afya njema na uhai mpaka wakati huo..

By Shafi_Abeid