Mikataba ya Polisi Yaitishwa Wizarani - MULO ENTERTAINER

Latest

7 Jun 2016

Mikataba ya Polisi Yaitishwa Wizarani

BAADA ya Rais John Magufuli kuizungumzia mikataba ya ujenzi ya Jeshi la Polisi iliyoingia na wawekezaji, Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ameitisha mikataba yote ya jeshi hilo.

Jeshi la Polisi nchini limetakiwa kuwasilisha mikataba ya miradi ya ujenzi wa nyumba za kuishi askari eneo la Kunduchi, Mikocheni pamoja na Kituo cha Polisi cha Oysterbay jijini Dar es Salaam pamoja na ule wa majengo mbalimbali ya mwekezaji ambaye Jeshi la Polisi limeingia mkataba naye.

Agizo hilo limetolewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Meja Jenerali Projest Rwegasira ikiwa ni miezi miwili tu tangu Rais Magufuli kuzungumzia mikataba hiyo na kuitilia shaka wakati akifungua kikao kazi cha makamanda wa Polisi wa mikoa, mawakili wafawidhi wa serikali wa mikoa na wakuu wa upelelezi wa mikoa na vikosi mjini Dodoma.

Meja Jenerali Rwegasira alisema mradi huo ni mkubwa na wa muda mrefu na hivyo ameliagiza jeshi hilo kuuwasilisha mkataba huo, ambao utekelezaji wake unaendelea ili aufahamu vizuri mkataba huo, unaolihusisha Jeshi la Polisi na Mwekezaji wa Kampuni ya Mara World Tanzania Limited.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo jana kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu huyo ametoa agizo hilo muda mfupi baada ya kukagua miradi hiyo katika maeneo ya Kunduchi na Mikocheni, ambako zinajengwa nyumba za kuishi askari wa Jeshi la Polisi na kwamba ujenzi wake bado unaendelea.

Mradi mwingine alioutembelea ni ujenzi wa Kituo cha Polisi eneo la Polisi Oysterbay na kuona maendeleo ya ujenzi huo sambamba na kufahamu hatua iliyofikiwa hadi sasa katika maeneo hayo ya Jeshi la Polisi.

Katika mradi huo wa Ujenzi wa Kituo cha Polisi Oysterbay, unaotekelezwa na mwekezaji Kampuni ya Mara World Tanzania Limited, pia kutajengwa ofisi za kukodisha, hospitali, maduka makubwa na hoteli.

Rais Magufuli wakati akihutubia makamanda hao wa Polisi Aprili mwaka huu, alisema miongoni mwa vitu ambavyo vinalisumbua jeshi hilo ni mikataba ya hovyo akisisitiza umuhimu wa fedha za jeshi hilo kutumika vizuri.

Rais Magufuli alisema kuna taarifa zinaonesha Jeshi la Polisi, limekuwa likihusishwa na matumizi mabaya ya fedha, hali inayoongeza ukubwa wa matatizo yanayokwamisha utendaji wake wa kazi.

Alitoa mfano wa taarifa za matumizi mabaya ya fedha, zinazotolewa kwa ajili ya kununua vifaa na sare za askari ama mikataba yenye mashaka inayotiwa saini kati ya Polisi na wawekezaji kuwa ni baadhi ya mambo yanayoongeza hali ngumu ya utendaji kazi kwa jeshi hilo.

“Oysterbay pale ni eneo ambalo ni zuri sana, kila mmoja anajua, mmeingia kwenye mikataba mnayoijua ninyi, mkapewa mtu anawajengea pale, sifahamu kama majengo hayo yanafaa.

“Palikuwa na ubaya gani eneo la Oysterbay likawa na hati, mkaitumia hiyo hati kwenda kukopa benki na kujenga nyumba hata za ghorofa 20 pale, mkaweka kitega uchumi na polisi wenu wakakaa pale?

“Nimesema lazima nizungumze kwa uwazi, nisiposema kwa uwazi nitajisikia vibaya nikimaliza mkutano huu. Nataka muelewe na muelewe ukweli mwelekeo ninaoutaka mimi,” alisema Rais Magufuli.