Trafiki Aliyetukanwa na Mke wa Waziri Apandishwa Cheo - MULO ENTERTAINER

Latest

28 Jun 2016

Trafiki Aliyetukanwa na Mke wa Waziri Apandishwa Cheo


Deogratius Mbango, askari wa kikosi cha usalama barabarani (trafiki) ambaye hivi karibuni alitukanwa na mke wa waziri wa serikali ya awamu ya tano (jina kapuni), baada ya kulikamata gari lake kwa kuvunja sheria za barabarani, hatimaye amepandishwa cheo ikiwa ni maagizo ya Rais Dk. John Magufuli.

Habari kutoka chanzo cha uhakika, zinasema kuwa askari huyo ambaye alilikamata gari la mke wa waziri huyo baada ya kuvuka sehemu ya waendao kwa miguu eneo la Namanga jijini Dar es Salaam, amepandishwa hatua moja mbele, kutoka koplo hadi sajenti.

Kitendo hicho cha kulikamata gari hilo, bila kujali utambulisho na matusi ya mwanamke aliyedai kuwa mke wa waziri, kilimfanya Rais Magufuli kumsifu na kumuona kuwa jasiri kazini kwake, hivyo kuliagiza jeshi la Polisi kumpa promosheni mara moja.

Juzi Jumapili, Uwazi lilimkuta trafiki huyo akiongoza magari maeneo ya Makumbusho katika lango la kuingilia daladala akiwa na cheo kipya cha usajenti.

Alipoulizwa kuhusu kuula huko, Mbango alikiri kutokea kwa jambo hilo na kumshukuru Mungu pamoja na uongozi wa Jeshi la Polisi kwa kumkumbuka, huku pia akilishukuru gazeti hili kwa kukumbushia katika toleo lake Na 993 lililoripoti juu ya kutotekelezwa kwa amri ya Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.