Sheikh Ponda Issa Ponda Amshukia Magufuli - MULO ENTERTAINER

Latest

7 Jul 2016

Sheikh Ponda Issa Ponda Amshukia Magufuli

KATIBU wa Jumuiya na Taasisi za Kiislam nchini (JTK), Sheikh Ponda Issa Ponda amesema, ni mapema mno kufurahia kauli ya Rais John Magufuli kuwa atarejesha mali za Waislam zilizoporwa na wajanja wachake. anaandika Mwandishi Wetu.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Sheikh Ponda amesema, “tunasubiri kuona utekelezaji wa kauli hiyo. Kama ni kweli imetoka moyoni, tutaiona.”

Hata hivyo, Sheikh Ponda amesema, “ipo mikataba mingi ya kifisadi iliyogharimu mali za Waislam. Nashukuru rais kutambua hilo na ikiwa atalitekeleza kwa vitendo, basi litakuwa jambo jema.”
Akizungumza katika Baraza la Eid lililoandaliwa na Baraza Kuu la Waislam Tanzania (Bakwata), kwenye viwanja vya Karimjee, jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alidai kuwa serikali yake itarejesha mikononi mwa waumini wa kiislamu mali zao zilizoporwa.
Alisema, kumekuwepo na malalamiko kwa taasisi hiyo kudhulumiwa mali zake na wafanyabaishara wajanja.

Alisema, “nakumbuka nilipokuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, viongozi wa Bakwata mlikuwa mnakuja ofisini kwangu kulalamika juu ya suala hili. Leo nimekuwa rais, nitazirejesha.”

Amesema, “niliwaambia wakati ule kwamba wanawadaganya, mnaingia nao ubia kumbe ni matapeli.”

Kutokana na dhamira hiyo, Sheikh Ponda amesema kuwa, yeye pamoja na Waislam wote wanapongeza hatua hiyo na wanasubiri kuona utekelezwaji wake.

“Mimi binafsi napongeza hatua hiyo, hatua ya kupitia mikataba ya kifisadi ni jambo jema. Kwa upande wetu, tupo tayari kutoa ushirikiano wowote unaohitajika.
“Tupo tayari kusaidia kutoa nyaraka zinazobeba ukweli juu ya jambo lililofanyika. Lengo letu ni kuona kile ambacho kimeporwa kinarejeshwa kwa wahusika.”
Akizungumzia hatua ya Rais Magufuli kutoa “ruzuku” kwa ajili ya kusaidia kusafirisha Waislam wanaokwenda kutekeleza ibada ya Hijja ambayo ni Nguzo ya Tano katika dini ya Kiislamu, Sheikh Ponda amesema, “ni fikra nzuri kusaidia katika Hijja.

Hata hivyo, Sheikh huyo machachari nchini anasema, “lakini naamini uhitajio mkubwa katika taasisi za dini ni kuboreshwa elimu na afya, siyo Hija.”

Anaongeza, “ingekuwa vizuri zaidi kama fedha hizo rais angezielekeza katika masuala ya kuboresha elimu na afya kwenye taasisi za Kiislam.”

Chanzo:Mwanahalisi