Madudu NSSF yaweka rehani ubalozi wa Dk Dau - MULO ENTERTAINER

Latest

29 Oct 2016

Madudu NSSF yaweka rehani ubalozi wa Dk Dau

Methali isemayo samaki mmoja akioza wote wameoza haisaili hali inayoendelea katika Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) ambako hadi sasa wakurugenzi sita na maofisa sita wako nyumbani kusubiri hatima yao kuhusu ushiriki wao kwenye miradi inayotiliwa shaka.

Wakati wakurugenzi hao wakiwa gizani kusubiri hatima yao, aliyekuwa mkurugenzi wao mkuu, Dk Ramadhani Dau  yuko Kualar Lumpa, Malaysia akiwakilisha nchi kama balozi.

Kwa kawaida, samaki mmoja akioza ni nadra kukuta wengine ndani ya tenga moja wakiwa hawajaharibika, na hata harufu huwa ni moja.

Lakini ni vigumu kutumia msemo huo kuelezea sakata hilo la NSSF kutokana na maofisa hao waandamizi kusimamishwa kutokana na miradi kadhaa ya ujenzi wakati bosi wao akipandishwa cheo kuwa balozi na baadaye kupelekwa Malaysia ambako anaendelea na kazi za kibalozi.

Dk Dau aliteuliwa kuwa balozi katika kipindi ambacho taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ikiwa imevuja kwenye vyombo vya habari, ikionyesha harufu ya ufisadi kwenye miradi ya shirika hilo kubwa ya hifadhi ya jamii iliyopo Kigamboni.

Alikuwa akiongoza kikao cha viongozi wa mikoa wa shirika hilo, lakini akaacha ghafla baada ya kupokea simu na kutoweka. Baadaye ilitangazwa kuwa ameteuliwa kuwa balozi.


Lakini, taarifa ya Ikulu ya Februari 15 haikueleza chochote kuhusu sakata hilo zaidi ya kusema atapangiwa kituo baadaye.

Wakati hali ikiwa haieleweki, Julai 15, wakurugenzi hao sita wa NSSF na mameneja watano na ofisa moja walitangazwa kusimamishwa kazi hadi uchunguzi wa masuala yanayohusu miradi ya ujenzi na ardhi itakapokamilika.

Lakini wakati hali ikiwa bado haijaeleweka, mwezi Septemba, Rais John Magufuli alitangaza kumpangia Dk Dau kituo cha kazi na baadaye kumuapisha tayari kwa kazi hiyo ya kuwa Balozi Malaysia.

Kwa kawaida, Mkurugenzi Mkuu wa shirika ndiye kiongozi wa vikao vya menejimenti vinavyohusisha wakurugenzi wote. Menejimenti ndiyo huhusika na uendeshaji wa shughuli za kila siku za shirika, ikiwa ni pamoja na miradi.

Mkurugenzi mkuu pia ni mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa shirika. Bodi hupanga na kutoa mwongozo wa shughuli zote za kibiashara na shirika.

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, mhadhiri wa zamani wa Chuo cha Diplomasia, Profesa Abdallah Safari alisema upo uwezekano kuwa Dk Dau aliachwa kwa makusudi wakati uchunguzi ukiendelea kufanywa dhidi yake.

Lakini, msemaji wa Serikali ambaye ni Mkurugenzi wa Habari (Maelezo), Hassan Abbas alisema: “Mashirika ya umma yana bodi zake. Watafutwe viongozi na Msajili wa Hazina ambaye mashirika yote yako kwake. Mimi siwezi kuzungumzia masuala ya shirika.”

Kati ya Januari na Februari kumekuwa na mgogoro wa malipo katika uwekezaji wa miradi iliyobuniwa na Bodi ya NSSF kwa ushirikiano na kampuni ya Azimio Housing Estate Limited (AHEL). Vibarua karibu wote walifukuzwa kazi baada ya kukosekana fedha za kuwalipa.

Baadaye iligundulika kuwa kampuni ya Azimio ilishindwa kutoa fedha kwa mujibu wa mkataba wa miradi ya ujenzi wa mji wa kisasa wa Dege Eco Village, Kigamboni, Dar es Salaam wenye thamani ya Dola za Marekani 653 milioni (Sh1.2 trilioni), na wa Arumeru, Arusha uliokuwa na thamani ya dola 3.34 bilioni (sawa na Sh7.2 trilioni).

Januari 21, NSSF na Azimio walilazimika kusitisha mradi wa Arumeru huku shirika likiwa limetoa Sh43.9 bilioni kwa ajili ya ushauri. Februari, mradi wa Dege ulisitishwa huku shirika likiwa limechangia Sh270 bilioni.

Matokeo tofauti

Dk Dau, ambaye amekuwa nembo ya mafanikio au kupanda na kushuka kwa shirika hilo, alipewa kazi mpya huku wakurugenzi sita na maofisa sita wakisimamishwa kazi kupisha uchunguzi kuhusu ushiriki wao katika miradi yenye kashfa.

Februari 15, Rais John Magufuli aliteua watu watatu kuwa mabalozi wapya, akiwemo Dk Dau hali iliyotafsiriwa kwamba anaondolewa katika nafasi ya mkurugenzi mkuu na kupewa cheo kikubwa. Wengine walioteuliwa ni Dk Asha-Rose Migiro na Mathias Chikawe na ilielezwa kwamba wangepangiwa vituo baadaye.

Machi 6 yaani siku 22 tangu Dk Dau aondolewe, lilifanyika jaribio la kujaza nafasi hiyo baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama kumtangaza Carina Wangwe, lakini uteuzi huo ulidumu kwa saa tano tu kabla ya kutenguliwa usiku.

Machi 18-31, mwaka huu, vyombo vya habari, likiwamo Gazeti la Mwananchi viliibua na kuripoti kwa kina ufisadi ulivyofanyika katika miradi ya NSSF;  kuanzia wa Dege, Mwanza, Mtwara hadi Arusha. Uozo ulihusisha makandarasi kulipwa fedha zaidi ya zilizoidhinishwa au kulipa mara mbili kwa kazi ileile.

Machi 19, Rais Magufuli alimteua Profesa Godius Kahyarara kuwa mkurugenzi mkuu mpya wa NSSF.

Aprili 19, wakati wa uzinduzi wa Daraja la Mwalimu Nyerere linalounganisha wakazi wa eneo la Kurasini na Kigamboni, Rais Magufuli alimsifu Dk Dau kwa ubunifu na usimamizi wa ujenzi wa daraja hilo ambalo alisema ni msaada mkubwa kwa wakazi wa Dar es Salaam.

“Watanzania huwa tunasahau sana, mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni,” alisema Rais Magufuli hali iliyotafsiriwa na wachambuzi wa masuala ya siasa kuwa alifurahishwa na utendaji wake.

Aprili 25, CAG, Profesa Mussa Assad aliwasilisha bungeni ripoti ikitia muhuri uchunguzi wa vyombo vya habari juu ya namna NSSF ilivyoingia ubia na kampuni binafsi ya Azimio isiyo na mtaji kujenga miradi mikoani Dar es Salaam na Arusha na ili kurahisisha kazi walianzisha kampuni ya Hifadhi Builders Limited.

Ripoti ya CAG ilionyesha udanganyifu katika mradi wa Dege. Azimio, iliyodai ina ekari 20,000 ilibainika kuwa na ekari 3,503 tu baada ya uchunguzi na hata ekari 300 ilizotoa katika awamu ya kwanza zilikuwa pungufu.

Vilevile, CAG alieleza kusikitishwa katika mradi wa Dege ambako ekari moja ilithaminishwa kwa Sh800 milioni huku katika mradi wa Arumeru ekari moja ilithaminishwa kwa Sh1.8 bilioni wakati wenyeji wanauza ekari moja chini ya Sh5 milioni.

Juni 29, Rais Magufuli alimteua Profesa Samwel Wangwe kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya NSSF.

Julai 18, Bodi ya Wakurugenzi ilitumia msemo wa bahati ya mwenzako usiilalie mlango wazi baada ya kutoa taarifa ya kuwasimamisha wakurugenzi sita na maofisa wengine sita kupisha uchunguzi juu ya ushiriki wao katika mradi wa ujenzi wa mji wa kisasa wa Dege Eco Village, Kigamboni ambako ripoti ya CAG ilionyesha ufisadi wa kutisha.

Waliosimamishwa ni Yakub Kidula (mipango, uwekezaji na miradi), Crescentius Magori (uendeshaji), Ludovick Mrosso (fedha), Chiku Mattesa (raslimali watu na utawala), Pouline Mtunda (ukaguzi wa ndani), Sadi Shemliwa (udhibiti athari), Amina Abdallah (meneja ununuzi), Chedrack Komba (meneja mkuu Kinondoni), Davis Kalanje (mhasibu mkuu), Abdallah Mseli (meneja miradi na uwekezaji), John Msemo (meneja miradi) na John Ndazi (ofisa umiliki).

Julai 19, mwenyekiti wa Bodi ya NSSF, Profesa Wangwe aliiambia Mwananchi kwamba hawezi kuzungumza lolote kuhusu hatima ya Dk Dau kwa vile si mwajiri wao.

“Bodi haiwezi kuchukua hatua dhidi yake, vyombo husika vitaamua kuhusu hilo,” alisema Profesa Wangwe.

Septemba14, Dk Dau aliapishwa kuwa Balozi wa Malaysia. Kuapishwa kwa Dk Dau na kisha kupangiwa kituo kulihitimisha minong’ono na mijadala katika mitandao ya kijamii kuhusu hatima ya mkurugenzi huyo.

Oktoba 26, Profesa Kahyarara aliiambia Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kuwa mradi wa Dege umesimama na wanahofia kupoteza Sh270 bilioni kutokana na kushirikiana na mbia ambaye hakuwa na fedha.

Profesa Kahyarara aliwaambia wajumbe kuwa mradi huo ulisimama tangu Februari na kwamba juhudi zinafanyika kuhakikisha mbia huyo AHEL anarejesha fedha.

“Tukitoka kwenye ubia huu tunaweza kupoteza fedha hizo tupo makini kuhakikisha mwekezaji huyo Azimio anarejesha fedha hizo,” alisema Profesa Kahyarara.

Wachambuzi

Akizungumzia hali hiyo, Profesa Abdallah Safari alisema: “Binafsi sioni kama ubalozi ni kupandishwa kutoka nafasi aliyokuwa nayo kama mkurugenzi wa shirika kubwa halafu kupelekwa kuwa balozi. Naweza kusema ameshushwa.

“Huenda wameona yeye ni mtu mzito ndiyo maana wakamtoa hapa ili uchunguzi uendelee labda uwepo wake ungeharibu.”

Mbunge wa Kaliua, Magdalena Sakaya alisema kitendo cha Dk Dau kuachwa hadi leo ni ishara serikali imeshindwa kuzingatia utawala bora.

“Ni heri basi angepelekwa mahakamani halafu ikathibitika hajahusika, lakini kuteuliwa kwake kwenda kuiwakilisha nchi nashindwa kuelewa kama kweli vita dhidi ya ufisadi inatekelezwa kwa haki,” alisema.

Mbunge wa zamani wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila alisema hicho ni kipimo kikubwa kwa Rais Magufuli katika vita yake dhidi ya ufisadi.

Kafulila alisema ufisadi wa NSSF ni zaidi ya ule wa Escrow na hatua hazichukuliwi kutokana na mfumo wa Serikali kuhusika katika hilo.

“Inavunja moyo kama ufisadi unaogusa mamlaka za juu za Serikali hauguswi, unaishia kuwatumbua watendaji wa chini,” alisema Kafulila.

“Watanzania wanasubiri kuona makali ya JPM katika hili. Kama ameamua kupambana kweli na ufisadi basi afanye hivyo kwa haki na usawa kwa wote bila kujali sura au uwezo. Wengine wanafukuzwa kazi bila hata kuhojiwa wakati Dau anapewa heshima ya ubalozi,” alisema.