Serikali Kuwabana Wanafunzi Wanaopewa Mikopo Kwa Kipaumbele - MULO ENTERTAINER

Latest

24 Oct 2016

Serikali Kuwabana Wanafunzi Wanaopewa Mikopo Kwa Kipaumbele

Serikali ipo katika mkakati wa kuwabana wanafunzi wanaopewa mikopo katika fani za kipaumbele, kutumikia katika utumishi wa umma nchini kwa muda fulani ili kuhakikisha dhamira ya serikali ya inatimia.

Fani hizo ni sayansi za tiba na afya, ualimu wa sayansi na hisabati, uhandisi wa viwanda, kilimo, mifugo, mafuta, gesi asilia, sayansi asilia, mabadiliko ya tabia nchi, sayansi za ardhi, usanifu majengo na miundombinu.

Serikali inachukua uamuzi huo, baada ya kubaini kuwapo wanafunzi wanaosomea fani hizo ili kupata mikopo, lakini baada ya kumaliza hukimbilia kufanya kazi nyingine au nje ya nchi na hivyo kuendelea kuwepo upungufu wa wataalamu waliowakusudia kubaki.

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na mafunzo ya ufundi, Stella Manyanya aliyasema hayo hivi karibuni, alipozungumzia utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu. Alieleza kuwa serikali inafikiria kuwe na utaratibu kwa wanaonufaika na mikopo ya kipaumbele kuingia makubaliano na serikali.

Alisema suala hilo halitakuwa jipya kwani hapo nyuma walikuwa wakibanwa kuwa lazima kufanya kazi angalau kwa miaka mitano serikalini na baadaye ni ruhusa kwenda popote, lakini kwa sasa hawawezi kuwabana wote, lakini lazima kufanya hivyo kwa hao wa kipaumbele.

Aidha Manyanya alizungumzia ulipaji mikopo hiyo na kudai wanaboresha sheria ya kukusanya madeni kwa kushirikiana na waajiri.

“Serikali itakusanya madeni hata kwa wakopaji ambao wamejiajiri kwa sababu wengi wakimaliza masomo hawafikirii kulipa,” alisema.”Sasa lazima walipe, wakopaji watambue fedha hizo ni mikopo na lazima kulipa.”

Alisema kwa wakopaji watakaoajiriwa, wizara inataka mkopo huo kuwa wa kwanza kukatwa kabla ya mingine ili kuepuka kuingiliana na sheria za kazi, zinazotaka mkopaji kuachiwa fedha fulani katika mshahara wake.