Wateule wa Magufuli Jifunzeni Kwake Katika Kuheshimu Michango ya Watu - MULO ENTERTAINER

Latest

19 Oct 2016

Wateule wa Magufuli Jifunzeni Kwake Katika Kuheshimu Michango ya Watu

Nampongeza Sana Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa uwezo wake mkubwa wa Kuheshimu Michango ya watu katika jambo fulani la kimaendeleo au tu la kijamii, nitatoa Mifano michache.

1. Wakati akiwa Waziri wa ujenzi Kule Hai eneo la Kwa Sadara palikuwa na Uzinduzi wa Barabara. Mgeni Rasmi katika shughuli ile alikuwa ni Rais wa Kipindi hicho Jakaya Mrisho Kikwete.

Wakati Magufuli anatoa neno la shukrani kama Waziri Muhusika, aliona Faida ya kumpa nafasi Mbunge wa Jimbo hilo Freeman Mbowe. Nina hakika waandaaji wa hafla Ile hawakumweka Mbowe kwenye ratiba lakini Magufuli aliheshimu uwepo wake na kuuthamini na kumkaribisha aseme kidogo.

2. Mwezi April mwaka huu 2016, tayari Akiwa Rais wa Nchi. Wakati wa Uzinduzi wa Daraja la Kigamboni, Rais alikuwa mtu wa mwisho kuzungumza, aliwasikiliza wote waliozungumza kabla yake, lakini hakuna hata mmoja aliyejaribu hata kutaja Jina la Mkurugenzi aliyestaafu wa NSSF Dkt. Ramadhani Kitwana Dau. Japokuwa ni Wakati wa Uongozi wa Dau ndio shirika hilo lilifanikiwa kugharamia sehemu kubwa ya ujenzi wa Daraja hilo.

Kabla hajazungumza. Rais alimuinua Dau, akamsifia na Kuheshimu mchango wake na Taasisi aliyoiongoza. Hakuna aliyeamini macho yake pale, kila mtu aliamini kuwa Rais akikutengua katika wadhifa na kukupangia wadhifa mwengine basi wewe ni mbadhilifu au Jipu, Dau akaogopwa, hakuwekwa kwenye Ratiba akihisiwa kuwa ni Jipu, Rais akauthibitishia Umma kuwa Dau hawezi kutenganishwa na ufanikishwaji wa Daraja lile.

3. Siku ya Uzinduzi wa Mradi mpya wa kupokea simu wa Jeshi la Polisi.
Rais aliwasikiliza wazungumzaji, wote walisahau kuwa Tukio lile lilifanyikia Kinondoni na Halimashauri ya Kinondoni ipo chini ya Upinzani ikiongozwa na meya Boniface Jacob.
Rais alimuita Meya aje kusalimia, Japo meya hakuwepo lakini aliheshimiwa.

4. Jana kwenye Kuaga Mwili wa Marehemu Masaburi, Rais aliona namna ambavyo sehemu kubwa ya wake wa Marehemu walivyotengwa na kutambulishwa mke mmoja tu . Rais akaweka Sawa kumbukumbu na kusisitiza Marehemu alikuwa na wake zaidi ya waliotajwa.
Mifano ni Mingi Mingi Mingi mno.

Leo inasambaa Video na taarifa inayoonyesha mgogoro wa kujitakia kabisa.
Mgogoro ambao Rais kila Mara amefanikiwa kuukwepa, Mgogoro wa Kuheshimu mchango wa mtu mwengine hata kama ni Mdogo.

Nimemuona Mbunge wa Arusha Mjini God bless Lema analalamika, analalamika Mkuu wa Mkoa wa Arusha kushindwa Kuheshimu mchango wake katika kufanikisha upatikanaji wa Mradi wa ujenzi wa Wodi ya wazazi mkoani humo.

Ukiiangalia vizuri ile video, unaweza kuwadharau wote wawili,
Unaweza kumdharau Lema analalamika kutokuwa recognized,
Lakini unaweza pia kumdharau Mkuu wa Mkoa kwa kushindwa kuona mchango wa kiongozi kijana mwenzake hata kama wanatofautiana itikadi.

Haingii akilini katika shughuli za kiserikali kuona viongozi wa mikoa na wilaya wa CCM na au vyama vingine wakiheshimiwa akadharauliwa Mbunge hata kama wa Upinzani.

Kulikuwa na shida gani kwa Gambo kumtaja Mbunge Lema hata kwa kuwepo kwake tu pale?,
Kulikuwa na ugumu gani kwa Lema kumsubiri Gambo Amalize ili athibitishe kuwa kuanzia mwanzo mpaka mwisho kuwa hakumtaja na amepotosha kama alivyodai? .

Nawaona pia vijana wakijadili swala hili katika msingi wa KI-UKAWA UKAWA na KI-CCM CCM,
hapana vijana wenzangu, hili ni zaidi ya vyama vyenu, hili ni jambo linalitutaka tutumie Busara zaidi kuliko Ushabiki.

Hakukuwa na haja ya kurumbana kwenye hili,
Hakukuwa na sababu ya kuonyeshana misuli, kwamba mimi ni Mbunge na Mimi ni Mkuu wa Mkoa.
Hakukuwa na haja ya viongozi wetu kuonyeshana tofauti zao hadharani, tena mbele ya wanaowaongoza na wafadhili wa Mradi huo.

Hakukuwa na sababu yoyote ya viongozi hawa kugombea Fito katika nyumba wanayoijenga wao wenyewe.
Ni Wakati Sasa wa wateule wa MAGUFULI kubadilika.
Too much is harmful.
Nawasilisha
Ndimi
Habib Mchange