Shehe Mkuu Dar: Diamond Acha Utani na Mungu - MULO ENTERTAINER

Latest

16 Jan 2017

Shehe Mkuu Dar: Diamond Acha Utani na Mungu

DAR ES SALAAM: Kufuatia kauli ya msanii mahiri wa muziki wa kizazi kipya Bongo, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kwamba kabla ya kuachia video zake huwa anasali rakaa mbili ndiyo maana huwa zinakubalika kwa watazamaji wake, Shehe Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhadi Mussa Salum amemjia juu na kumtaka kuacha utani na Mungu.


Kwa kauli yake, wakati akihojiwa na kituo kimoja cha runinga, Diamond alisema huwa anafanya maombi maalum usiku kwa kuswali rakaa mbili kabla ya kuachia video yoyote, jambo alilosema kwamba ndiyo siri ya mafanikio yake.

“Unajua mimi huwa nafanikiwa kwa kiasi kikubwa kwenye video zangu kwa sababu huwa nasali rakaa mbili usiku na kumuomba Mungu ili nifanikiwe kwa video nzuri, nashukuru Mungu anasikia maombi yangu,” alisema Diamond.


Amani lilipomtafuta Shehe Alhadi na kumuuliza kama alichokisema Diamond kina mashiko yoyote kidini, alisema katika dini ya Uislam, muziki wa kidunia ni dhambi na haukubaliki ndiyo maana wasanii kama Mzee Yusuf, wameamua kujiweka nao mbali kwa sababu ni kumkosea Mwenyezi Mungu.

Akaongeza kuwa, alichokisema Diamond ni kama kumfanyia Mungu utani kwa sababu huwezi kuswali, ukamuomba baraka zake ili uende kufanya jambo ambalo ni chukizo mbele zake. Akasema dua za namna hiyo huwa hazipokelewi na Mungu na yeyote anayefanya hivyo, huzidi kumkosea Mungu.

Shehe mwingine aliyezungumza na gazeti hili kwa masharti ya kutochorwa jina gazetini, alisema anachokifanya Diamond ni sawa na mtu ambaye anamuomba Mungu kabla ya kwenda kuiba, jambo ambalo ni tofauti kabisa na misingi ya dini.