Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli
amemkabidhi Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa kazi ya kuzuia na
kupambana na dawa za kulevya akiwa kama Mwenyekiti wa Tume ya Kudhibiti
Dawa hizo nchini.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati
akiwaapisha Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji, Anna Peter Makakala,
Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya,
Rogers William Sianga pamoja na mabalozi watatu Mhe. Omary Yusuph Mzee,
Mhe.Joseph Edward Sokoine pamoja na Mhe. Grace Aron Mgovano aliowateua
hivi karibuni.
Dkt. Magufuli amesema kuwa Waziri Mkuu anatajwa kwenye Sheria Na.5 ya
mwaka 2015 kuwa ni Mwenyekiti wa Tume hiyo ambapo Wajumbe wake ni Waziri
wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Waziri wa Mambo ya Ndani, Waziri wa
Elimu ana Mafunzo ya Ufundi, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo, Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Waziri wa
Fedha na Mipango, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto pamoja na Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
“Nalipongeza sana Bunge la kipindi cha mwaka 2010 – 2015 chini ya Spika
mstaafu, Mhe. Anne Makinda lililopitisha Sheria hii baada ya kuona
sheria za mwanzo za kupambana na dawa za kulevya hazina nguvu hivyo
Wabunge wa wakati ule walisimama kwa pamoja bila kujali itikadi za vyama
vyao wakapitisha sheria hii,” alisema Dkt. Magufuli.
Aidha, Dkt. Magufuli amempongeza Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete kwa
kusaini sheria hiyo haraka mara baada ya Bunge hilo kuipitisha kwa
sababu alijua madhara ya dawa za kulevya katika nchi yetu.
Amefafanua kuwa sheria imeeleza wazi katika kifungu cha 10 cha Sheria
Na.5 ya mwaka 2015 kuwa jukumu la kupambana na dawa za kulevya
linasimamiwa na Serikali pekee yaani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Makamo wa Rais,
Waziri Mkuu, Mawaziri, Wakuu wa Mikoa na Wilaya pamoja na Wakurugenzi wa
Halmashauri za Wilaya au mtu yoyote atakayekuwa amepewa mamlaka ya
kusimamia Serikali.
Kwa upande wake Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa amesema kuwa Taifa
limeendelea kushuhudia kizazi chetu kikiendelea kudidimia kwa sababu ya
matumizi ya dawa za kulevya na Serikali kwa mipango yake imeendelea
kukemea, kudhibiti na kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya wazalishaji,
wasambazaji, wauzaji na watumiaji wa dawa hizo.
“Jambo hili limeleta athari kubwa sana kwani vijana wetu wengi
wamepoteza uwezo wa kujisimamia katika shughuli zao za maendeleo kwa
sababu baada ya matumizi tumeona athari kadhaa zikiwezo za kudhoofishwa
kwa mwili, uwezo wa kutafakari pamoja na kutoweka kwa uwezo wa kufanya
kazi,”alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri Mkuu Majaliwa ameongeza kuwa Taifa hili la Watanzania kwa kiasi
kikubwa linawategemea vijana waweze kuleta msukumo wa maendeleo ndani ya
nchi hivyo jambo hili likiachiwa linaweza kuleta athari kubwa katika
ukuaji wa uchumi na maendeleo yetu kwa ujumla wake.
Alisisitiza kuwa vita hii ilianza, inaendelea na itaendelea kupiganwa
hadi imalizike hivyo Watanzania hawana budi kuunga mkono jitihada zozote
zinazofanywa na Serikali kuhakikisha wanatokomeza uzalishaji,
usambazaji, uuzaji na matumizi yake kwa namna yoyote ile, kila mmoja
anatakiwa kushiriki kikamilifu ili kubaini matumizi ya dawa za kulevya
ndani ya nchi hii.