KATIBU Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, amesisitiza kuwa haoni
sababu ya kukutana na Profesa Ibrahim Lipumba kuzungumzia mambo ya chama
kwa kuwa si mwanachama halali wa CUF hivi sasa.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, ilisema
Maalim Seif alitoa kauli hiyo kwenye ziara ya siku nne kwenye wilaya
saba za mikoa mitatu ya Unguja.
Maalim alisema ataendelea kufuata taratibu za kisheria ili kuhakikisha
chama kinamaliza moja kwa moja mgogoro aliodai umepandikizwa na CCM
kupitia kwa Lipumba.
Alitaka wapenzi na wanachama wa CUF kuunga mkono jitihada zinazofanywa na chama kupigania demokrasia ya kweli nchini.
Aliwataka wanachama wa CUF kushirikiana na viongozi wakuu wa CUF
wanaotambuliwa na Baraza Kuu la Uongozi kujenga na kuimarisha chama
hicho.
Alifafanua kuwa wakati anaendelea kuimarisha chama kupitia viongozi
halali, ni vema wasiwe na wasiwasi na uamuzi walioufanya kwenye uchaguzi
mkuu wa Oktoba 25 mwaka juzi kwa kuipa CUF ushindi wa urais wa Zanzibar
kuwa hautapuuzwa.
Aliwataka kuendelea kuwa watulivu na kuwahakikishia kuwa siku chache
zijazo haki yao itapatikana. "Nawahakikishia, tumepigana vya kutosha
katika kudai haki yetu na tumefikia hatua nzuri za kupata haki yenu.
“Hatua ya wananchi wa Zanzibar ya kuipa ushindi CUF ni kutokana na CCM
kushindwa kuongoza Wazanzibari kwa misingi ya haki, usawa na
demokrasia,” alisema.
Alifafanua kuwa mgogoro wa uongozi ndani CUF uliotokana na hatua ya
Profesa Lipumba kuamua kurudi katika nafasi ya uenyekiti wa chama hicho
na kusema watahakikisha wanapata ushindi.
“Lipumba alijiuzulu mwenyewe hivyo hakuna hoja yoyote ya kisheria inayomwezesha kurudi tena katika nafasi hiyo,” alisema.
Maalim Seif ataendelea na ziara hiyo katika Wilaya ya Magharibi ‘A’, ‘B’ kisiwa cha Unguja, Pemba hadi Februari 24.
Pamoja na kufanya ziara hiyo na kuzungumza na viongozi wa chama na
jumuiya zake, Katibu atafanya uzinduzi na uimarishaji wa waratibu wa
chama.