MKUU wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Simon Sirro,
amesema watu wanaotumwa kutekeleza mauaji Wilaya za Kibiti, Mkuranga na
Rujifi watajibiwa kwa ubaya na kwamba kuanzia sasa wametangaza vita
dhidi yao.
Alisema watu hao ambao wanaua raia na askari walidhani watawachonganisha
wananchi kirahisi bila kujua Watanzania wana umoja usioweza
kugawanyika.
Sambamba na hilo, amesisitiza kuwa suala la ulinzi ni la watu wote na
kwamba wananchi wa maeneo hayo wanapaswa kujilinda kwa kuanzisha vikundi
vya ulinzi shirikishi.
IGP Sirro aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam, wakati akipokea
msaada wa magari manne kila moja likiwa na thamani ya Sh. milioni 126.2
kutoka kampuni ya Haval Great Wall Motors, yatakayosaidia kupatamba na
uhalifu nchini.
“Sisi Tanzania hatujazoea vurugu za namna ile kwa hiyo wale ambao
walikuwa wametumwa walifikiria Tanzania kama nchi nyingine wataona
majibu yake,” alisema.
“Tangu zamani sisi ni wamoja na tunapendana kwa hiyo wale waliokuwa
wametumwa vibaya vibaya na sisi tutawajibu kwa ubaya ubaya tu.”
Alisema Jeshi la Polisi linakwenda vizuri na suala la mauaji ya Kibiti na kwamba muda si mrefu kutakuwa na majibu mazuri.
IGP Sirro ambaye aliapishwa na Rais John Magufuli Mei 29, mwaka huu,
akichukua nafasi ya Ernest Mangu aliyeondolewa, alisema wenyeviti wa
vijiji wa Mkoa wa Pwani wana wajibu wa kuimarisha hali ya ulinzi katika
maeneo yao.
“Maeneo hayapitiki, Kibiti, Ikwiriri, Mkuranga hata maeneo mengine ya
nchi wananchi wanapaswa kujilinda kwa kuanzisha ulinzi shirikishi,”
alisema IGP Sirro.
Alisema matukio ya uhalifu kwa miaka ya sasa yamekuwa magumu kuliko ya
miaka ya nyuma, hivyo jeshi hilo linapaswa kwenda na wakati.
Kwa mujibu wa Sirro, Jeshi la Polisi linakabiliwa na changamoto
mbalimbali kama vile uhaba wa vitendea kazi, ufinyu wa bajeti na uwapo
wa miundombinu mibovu ambayo ni kikwazo kwa polisi kufika sehemu ya
tukio kwa haraka.
Naye Meneja wa kampuni iliyotoa magari hayo, Jianguo Liu, alisema
wametoa msaada wa magari hayo kwa Jeshi la Polisi kwa lengo la kusaidia
kupambana na uhalifu.
Mauaji katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani yalianza
Januari, 2015 idadi ikitajwa kufikia 39 huku wanaotekeleza mauaji hao
wakiwa hawafahamiki.
Mauaji ya mwisho kutekelezwa yalitokea Juni 27, mwaka huu, wilayani
Kibiti baada ya watu wawili kuuawa kwa kupigwa risasi katika kijiji cha
Mangwi, kata ya Mchukwu wilayani Kibiti usiku, huku mtu mmoja
akijeruhiwa vibaya sehemu ya jicho.
Mauaji hayo yalitekelezwa ikiwa imepita wiki moja baada ya askari wawili
wa usalama barabarani wilayani Kibiti mkoani Pwani kuuawa kwa kupigwa
risasi katika kijiji cha Masafiri kata ya Bungu, huku askari mmoja
akisalimika.
Moja ya matukio yaliyowahi kutokea wilayani Kibiti Mkoa wa Pwani na
kuacha historia kwa Jeshi la Polisi ni lile lililotokea Aprili 13, mwaka
huu, baada ya askari wanane kushambuliwa wakitoka kubadilishana lindo.
Katika shambulio hilo, majambazi hao walipora bunduki saba ambazo ni SMG nne na Long Range tatu zikiwa na risasi zake.
Kutokana na mwendelezo wa mauaji katika Wilaya hizo, IGP Sirro
alipoingia madarakani alitangaza donge nono la Sh. milioni 10 kwa mtu
yeyote atakayefanikisha kutoa taarifa za kukamatwa kwa watuhumiwa 12 wa
mauaji.
Watuhumiwa hao ni pamoja na Abdurshakur Ngande Makeo, Faraj Ismail
Nangalava, Anaf Rashid Kapera, Said Ngunde, Omary Abdallah Matimbwa,
Shaban Kinyangulia, Haji Ulatule, Hassan Uponda, Rashid Salim Mtulula,
Hassan Nasri Mzuzuri na Hassan Njame.
IGP Sirro alitangaza bingo hiyo zikiwa zimepita siku chache tangu
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Onesmo Lyanga alipotangaza bingo
ya Sh. milioni tano kwa yeyote atakayetoa taarifa zitakazowezesha
kukamatwa kwa watu hao.
POLISI KUWEZESHWA
Wakati huo huo, Serikali imesema imeongeza doria na vitendea kazi kwa
Askari wa Mkoa Maalum wa Kipolisi wa Rufiji unaoundwa na wilaya za
Mkuranga, Kibiti na Rufiji mkoani Pwani.
Katika hotuba yake ya kuahirisha Bunge jana, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
alisema pia tayari Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo maalum ameshateuliwa
na kutoa rai kwa wananchi wa maeneo hayo kutoa ushirikiano kwa serikali
ili kuwezesha watuhumiwa wote kukamatwa.
Majaliwa alisema dhamira ya serikali ni kuhakikisha kila raia wa
Tanzania, wakiwamo wananchi wa wilaya hizo, wanakuwa huru kufanya
shughuli zao za maendeleo bila kuhofia usalama wa maisha yao.
“Serikali inaendelea kuchukua hatua za muda mfupi na za muda mrefu ili
kurejesha hali ya usalama katika maeneo hayo. Tumeongeza doria na
vitendea kazi kwa askari,” alisema Majaliwa.
6 Jul 2017
New
mulo
SIRRO