Raila Odinga Bado Kichwa Ngumu...Hajakubali Kushindwa Uhuru Kenyatta...Sasa Kuchukua Maamuzi Haya - MULO ENTERTAINER

Latest

17 Aug 2017

Raila Odinga Bado Kichwa Ngumu...Hajakubali Kushindwa Uhuru Kenyatta...Sasa Kuchukua Maamuzi Haya

Kiongozi wa upinzani nchini Kenya Raila Odinga ametangaza kwamba muungano wake wa National Super Alliance utawasilisha kesi mahakamani kupinga ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta katika uchaguzi mkuu uliofanyika Jumanne wiki iliyopita.

Bw Odinga alikuwa amesema ingawa muungano huo ulikuwa umeapa kutowasilisha kesi kortini wakati huu, wameona ni heri kufanya hivyo "kufichua uovu uliotokea wakati wa uchaguzi mkuu."

"Tumeamua kwenda kortini kufichua jinsi uongozi wa kompyuta ulivyofanikishwa," amesema Bw Odinga akiwahutubia wanahabari mtaa wa Lavington, Nairobi.

"Hawa ni viongozi wa kompyuta. Kompyuta ndiyo iliwataga, kompyuta iliangulia, kompyuta iliwatoa. Vifaranga vya kompyuta."

Kiongozi huyo amesisitiza msimamo wa NASA kwamba uchaguzi haukuwa huru na wa haki.

Amesema mitambo ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi IEBC ilidukuliwa na matokeo kuvurugwa kumfaa Bw Kenyatta ambapo kulikuwa na pengo kiasi fulani kati yake na Bw Odinga muda wote wa kutangazwa kwa matokeo.

"Mtindo huu ulitokea pia katika maeneo mengi uchaguzi wa ugavana. Jambo kama hili halijawahi kutokea katika uchaguzi wa kidemokrasia pahala pengine popote duniani. Lakini ilitokea hapa," alisema.

Bw Odinga amesema udukuzi huo una uhusiano na kuuawa kwa meneja wa teknolojia katika tume hiyo Chris Msando ambaye aliuawa wiki moja kabla ya uchaguzi.
Samahani, kisakuzi chako hakiwezi kuonesha ramani hii

Aidha, kiongozi huyo ameishutumu tume ya uchaguzi akisema imekuwa ikitangaza matokeo ya uchaguzi bila kutoa Fomu 34A za kuonyesha matokeo yalivyokuwa katika vituo vya kupigia kura.
Bw Odinga mesema uchunguzi wa muungano huo umebaini udanganyifu mwingi ulitokea, na akawashutumu waangalizi wa uchaguzi ambao walisema uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.

Waziri mkuu huyo wa zamani amesema upinzani uliwasilisha kesi mahakamani kupinga matokeo mwaka 2013 lakini hawakutendewa haki, na kusema "Uhuru (Kenyatta) alishinda 100%, nasi tukashindwa 100%."

"Mahakama inaweza kutumia hii kama nafasi ya pili ya kujitakasa, au inaweza kuamua kuharibu mambo kabisa," amesema.

Jamii ya kimataifa ilikuwa imehimiza upinzani, pamoja na wagombea wengine ambao hawakuwa wameridhishwa na uchaguzi, kutumia mifumo iliyowekwa kikatiba kutafuta haki.

Kwa mujibu wa matokeo ya IEBC, Rais Kenyatta alipata kura 8,203,290 huku naye Raila Odinga akipata kura 6,762,224.