Waziri Majaliwa Atoa Agizo kwa Wakuu wa Mikoa - MULO ENTERTAINER

Latest

10 Sept 2017

Waziri Majaliwa Atoa Agizo kwa Wakuu wa Mikoa

Majaliwa Atoa Agizo kwa Wakuu wa Mikoa
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa 10 inayolima pamba nchini kusimamie zao hilo kwa karibu ili kuinua uzalishaji wake na kuwaongezea kipato wananchi.

Majaliwa alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na wakuu hao wa mikoa kwenye kikao alichokitiisha mjini Dodoma, kujadili mbinu za kufufua zao hilo.

Wakuu wa mikoa waliohudhuria kikao hicho ni kutoka Shinyanga, Singida, Kagera, Tabora, Morogoro, Mara, Mwanza, Simiyu, Katavi na Geita.

“Serikali imeamua kufufua mazao makuu matano ya biashara ambayo ni pamba, chai, kahawa, korosho na tumbaku na leo (jana) nimetaka nianze na ninyi wakuu wa mikoa ili mwende mkawasimamie watu wenu tunapokaribia kuanza msimu mpya,” alisema.

Majaliwa alisema Serikali imeamua kusimamia kilimo cha pamba kuanzia maandalizi ya shamba, kupanda, matumizi ya pembejeo na dawa, kuvuna na kutafuta masoko na akawataka wasimamie katika maeneo yao ili kilimo cha zao hilo kiweze kubadilika.

“Kama hajafanya kazi hiyo, usiridhike kuwa na ofisa kilimo wa aina hiyo,” alisema Majaliwa na kuongeza:

“Lazima kila mmoja awe na mpango kazi, ausimamie na atoe matokeo ya kuwa zao hili limefanikiwa katika eneo lake. Tunataka zao hili lichukue nafasi yake ya namba moja. Heshima ya “Dhahabu Nyeupe” lazima irudi lakini pia ni vyema mkumbuke kuwa zao la pamba ni uchumi, zao la pamba ni siasa katika mikoa yenu.”

Wakulima wa pamba wamekuwa wakilalamikia bei kubwa ya pembejeo ambazo husambazwa na mawakala, huku wakipewa baada ya mavuno wakipewa bei ambayo hailingani na gharama za uzalishaji.

Pia, wamekuwa wakilalamikia kuuziwa mbegu ambazo hazioti na hakuna fidia ambayo hulipwa.