Rais mtaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ameishauri Serikali kuandaa utaratibu endelevu utakaosaidia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya Ukimwi.
Mkapa amesema hayo jana wakati akizindua harambee ya kuchangia Mfuko wa Ukimwi iliyoandaliwa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (Tacaids).
Mkapa amesema wafadhili wamepunguza misaada ya Ukimwi, hivyo fedha za ndani ni muhimu ili kupunguza utegemezi.
“Naipongeza Serikali kwa kuendelea kuchangia fedha kupitia bajeti zake, hata hivyo nashauri uwekwe utaratibu endelevu utakaosaidia kupata fedha za Ukimwi,” amesema
Amesema kwa kutumia fedha za ndani zitasaidia wagonjwa wa Ukimwi kuwa na uhakika wa kupata matibabu.
Akitoa mfano, amesema mwaka 2017/18 mahitaji kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo yalikuwa Sh1.2 trilioni, lakini fedha zilizoahidiwa na wafadhili ni Sh740 bilioni na upungufu ulikuwa Sh520 bilioni.
“Wafadhili wamepunguza misaada ya Ukimwi, tunapaswa kutafuta vyanzo vya mapato vya ndani ili kuziba pengo hilo,” amesema Mkapa ambaye kipindi cha utawala wake ndiye aliyeutangaza ugonjwa huo kuwa janga la kitaifa mwaka 1999.
Amesema ipo haja ya wadau kushirikiana na Serikali katika kuuchangia mfuko huo ili uweze kuhudumia wagonjwa.
Pia, aliziomba taasisi na mashirika ya umma kuchangia mfuko huo kwa kuwa bila kuwa na watu wenye afya njema Taifa halitapiga hatua za maendeleo.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama amesema fedha zinazochangwa kwa ajili ya mfuko huo ziko salama.
Amesema mfuko huo umeweka mwongozo wa namna ya kutumia fedha hizo ili kuondoa matumizi yasiyokuwa ya lazima.
Akifafanua, amesema mwongozo huo unaonyesha kuwa asilimia 60 ya fedha zinazokusanywa na mfuko hutumika kwa ajili ya ununuzi wa dawa za kufubaza makali ya virusi vya Ukimwi (ARV).
Mhagama amesema asilimia 25 ya fedha za mfuko huo hutumika kwa ajili ya huduma za kinga na usambazaji wa kondomu pamoja na utoaji wa elimu, wakati asilimia 15 hutumika kwa ajili ya uwezeshaji, ufuatiliaji na tathmini ya Ukimwi.
“Hivyo nawahakikishia wadau kwamba fedha mnazochangia kwa ajili ya mfuko huu ziko salama na zinatumiwa kwa malengo yanayokusudiwa,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mfuko wa Ukimwi (ATF), Godfrey Simbeye amesema hauwezi kutosheleza mahitaji yake kwa kutegemea uchangiaji wa harambee.
Pia, amesema wakati umefika wa kutafuta vyanzo vingine vya mapato ili viweze kusaidia katika mapambano dhidi ya Ukimwi.
“Kuna wataalamu wanaandika andiko ambalo litapendekeza kwa Serikali ili tuwe na tozo la Ukimwi kwenye manunuzi, hilo likifanikiwa tutakuwa tumepiga hatua kubwa,” amesema.