Polisi wa kitengo maalumu cha kupambana na ufisadi (Hawks) wamethibitisha kwamba watu watatu wamekamatwa baada ya kuvamia mapema asubuhi makazi ya familia tajiri ya Gupta yaliyopo eneo la Saxonwold jijini hapa.
Pamoja na kuthibitisha kukamatwa watu hao, msemaji wa Hawks, Hangwani Mulaudzi hakutaka kuweka wazi majina ya waliokamatwa.
"Hebu tuseme tu kwamba mashtaka yao yanahusu udanganyifu," amesema.
Inaaminika kwamba kabla ya kuvamia makazi ya Gupta, maofisa wa Hawks walikuwa wamevamia kwanza makazi ya Bedfordview yanayoaminika kuwa ya Mkurugenzi mtendaji wa zamani wa kampuni ya Sahara Systems. Mulaudzi alikataa kutoa maoni ikiwa matukio mawili hayo yana uhusiano.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kwamba Hawks pia walivamia ofisi za kampuni ya Oakbay ya Gupta zilizopo mjini Sandton Jumatano asubuhi.
Kwa mujibu wa mlinzi ambaye hakutaka jina lake litajwe, maofisa wa Hawks waliwasili wakiwa kwenye magari matatu karibu 1:30 na wakaingia ndani ya jengo hilo. Waliondoka muda mfupi baadaye, walinzi alisema.
Akina Gupta ambao ni familia tajiri ya wazaliwa wa India wamekuwa wakishutumiwa kwa kutumia urafiki wao na Rais Jacob Zuma kwa manufaa binafsi na kibiashara. Familia hiyo ndiyo inatuhumiwa kuiweka Serikali mfukoni katika kashfa kubwa ya ufisadi.
Familia hiyo inayomiliki baadhi ya biashara nchini Afrika Kusini imeshutumiwa kutumia vibaya ushawishi wao na urafiki na Zuma kupata mikataba ya Serikali inayogharimu mamilioni ya dola za Kimarekani.
Mapema, Shirika la TimesLIVE liliripoti kuwa familia ya Gupta inayopigwa vita ilikuwa inataka kuingia makubaliano maalumu na Hawks. Habari kuhusu mpango huo zilivuja baada ya ripoti kwamba mwana wa Rais Jacob Zuma na mshirika wa biashara wa familia ya Gupta, Duduzane Zuma alikuwa amejiandaa kujipeleka pamoja na wanasheria wake kwa Hawks Jumatano.
Duduzane, akijibu ujumbe aliotumiwa na simu alizopigiwa alisema alikuwa katika mkutano, hivyo hawezi kuzungumza.