Siku 12 tangu Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ alipoachiwa huru, jana aliingia bungeni na kusimamisha shughuli za Bunge kwa dakika kadhaa.
Sugu, ambaye ni mbunge wa Mbeya Mjini (Chadema), alihudhuria kikao cha 33 cha Bunge la Bajeti lililoanza Aprili 3 likitarajiwa kuhitimishwa Juni 29 akiwa amevaa suti ya bluu bahari ikiwa na nembo ya namba yake ya mfungwa 219/2018.
Akiwa ameongozana na mbunge wa viti maalumu (Chadema), Kunti Yusuph, Sugu alikanyaga lango la kuingia bungeni saa 3:16 asubuhi kabla ya kuingia ukumbini saa 3:20.
Wakati akiingia, mbunge huyo alipita katikati ya ukumbi na wabunge wa upinzani walianza kumshangilia kwa kugonga meza. Awali alikosa vikao vya Bunge tangu Novemba, mwaka jana.
Wa kwanza kusalimiana na mbunge huyo alikuwa mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye kisha akapokewa na mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini kwa upande wa upinzani.
Wakati Sugu akiingia bungeni, naibu waziri wa Tamisemi, Josephat Kandege alikuwa akijibu maswali ya wabunge lakini alilazimika kusubiri kwa muda kabla ya Sugu kuhamia upande wanapokaa wabunge wa CCM na mawaziri.
Kisha baada ya salamu hizo, Sugu alisalimiana na waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Kazi na Watu wenye Ulemavu, Jenista Mhagama; mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Adelardus Kilangi na waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora), George Mkuchika.
Wakati anarudi upande wake wa upinzani, Sugu alimpigia saluti mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge kisha akakumbatiana na Selasini na kwenda kukaa sehemu yake karibu na mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko ambaye alimpa vitabu vya hotuba za wizara zilizopita.
Kutokana na shangwe, mwenyekiti wa Bunge, Chenge alisema hatawapa wabunge nafasi ya kuuliza maswali ya nyongeza jambo lililozidisha shangwe ukumbini.
Kwa kuwa kipindi cha maswali na majibu kilikuwa kikiendelea, Chenge alimpa nafasi Sugu ya kuuliza swali la nyongeza ndipo alipoitaka Serikali kuangalia upya baadhi ya sheria akisema ni mbovu na hazifai kutumika kwa sasa.
Mbunge huyo aliitaja Sheria ya Huduma ya Habari akisema inakwenda kinyume cha Katiba ya nchi ibara ya 18.
“Mfano mimi nilifungwa kutokana na kuzungumza na wananchi wangu kuhusu watu kupigwa risasi, kuokota maiti kwenye viroba na demokrasia ya nchi,” alisema Sugu.
Akijibu swali hilo, naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Elias Kwandikwa alisema sheria zote hutungwa na Bunge, hivyo kwa kuwa mbunge huyo amerudi bungeni ipo haja ya kukutana na kujadiliana kuona namna ya kufanya.
Kabla ya kujibu swali hilo, Kwandikwa alimkaribisha Sugu akisema, “Kwanza nikukaribishe sana hapa bungeni, karibu sana mheshimiwa Mbilinyi.”
Mapema, mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea alitaka kujua ni lini Serikali itapeleka bungeni muswada wa kuifanyia marekebisho sheria inayobana uhuru wa mwananchi wa kupata habari.
Kwandikwa alisema Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 13 ya mwaka 2015 ni adhimu kwa kuwa inaainisha makosa na adhabu dhidi ya uhalifu unaotendeka mtandaoni.
Alisema sheria hiyo inaweza kuimarika kwa matumizi salama ya mtandao kama vile Serikali mtandao, elimu mtandao, biashara mtandao na hivyo kuleta maendeleo.
Alipokuwa amekaa Sugu, wabunge wa upinzani hawakukatika kwenda kuzungumza naye na kuitazama nembo iliyokuwa upande wa kushoto wa kifua chake.
Azungumzia namba yake
Akizungumza na Mwananchi kuhusu nembo hiyo baada ya kikao cha Bunge, Sugu alisema, “Hii ni namba yangu (219/2018) halisi ya mfungwa niliyokuwa naivaa gerezani.”
Alisema ataendelea kuivaa na baadaye ataiweka kwenye maktaba yake nyumbani.
Akizungumzia mapokezi ndani ya Bunge alisema, “Nimefarijika sana. Imeonyesha wabunge wenzangu pia hawakufurahishwa na walisikitishwa na kufungwa kwangu. Tena wabunge hata wa CCM.”
Baada ya kutoka ukumbini alisalimiana na kuteta na wabunge akiwamo waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi.
Magereza wafafanua
Akizungumzia uamuzi wa Sugu kuivaa namba hiyo uraiani, ofisa habari wa Jeshi la Magereza, Lucas Mboje alisema huo ni uamuzi na utashi wa mhusika na haihusiani na jeshi hilo.
“Sisi tumemalizana naye, kwa sasa sio mteja wetu. Huo ni utashi wake mwenyewe Sugu,” alisema Mboje
22 May 2018
New
mulo
SUGU