Martha Mboma na Sweetbert Lukonge
KOCHA Msaidizi wa Simba, Selemani Matola, ameomba kuondoka klabuni hapo ikiwa ni siku chache tangu timu hiyo ilipofungwa na Mbeya City mabao 2-1 katika Ligi Kuu Bara kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Matola ambaye alianza kuifundisha timu hiyo msimu uliopita akisaidiana na aliyekuwa kocha mkuu wa klabu hiyo, Zdravko Logarusic, ameomba kuondoka baada ya kuwepo kwa maneno mengi juu ya uwepo wake katika benchi ya ufundi akiwa chini ya Goran Kopunovic.
Rais wa Simba, Evans Aveva ndiye ambaye ametoa kauli juu ya taarifa hiyo na kukiri kuwa wamepokea barua ya Matola akiomba kuachia ngazi juzi.Aveva amesema kuwa katika barua hiyo, Matola ameomba kupunguziwa majukumu na kupewa mengine au kuondoka kabisa klabuni hapo baada ya kukabiliwa na matatizo mbalimbali yakiwemo ya kifamilia ambayo yanamfanya ashindwe kufanya kazi yake kwa ufanisi mkubwa.
Aveva amesema kuwa uongozi wa Simba unamuamini Matola na amekuwa mtumishi mzuri klabuni hapo kwa muda mrefu na kusisitiza kuwa wao hawana tatizo naye.
“Matola alileta barua yake jana (juzi) jioni ya kuomba kupunguziwa majukumu kwa kupewa kazi nyingine au kuachana kabisa na klabu kutokana na kukabiliwa na masuala ya kifamilia.
“Hatujatoa tamko lolote, tutakutana na kamati ya utendaji kuweza kujadiliana kujua nini cha kufanya,” alisema Aveva.
Aidha, Aveva aliongeza kuwa, mkutano mkuu wa klabu hiyo, unatarajiwa kufanyika Machi Mosi, mwaka huu baada ya awali kutofanyika kutokana na kuingiliana na Kombe la Mapinduzi.Alipoulizwa Matola jana kuhusiana na ishu hiyo alisema: “Ni kweli lakini nipo njiani, naelekea mazoezini, kwa hiyo siwezi kuizungumzia kwa sasa.”
31 Jan 2015
New
mulo
News