New
TENDO cha wanafunzi wa vyuo vikuu kunyimwa mikopo huku wachache waliopewa wakipunguziwa fedha za kujikimu kimeichukiza Serikali ya Wanafunzi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (DARUSO) na kuamua kuwazuia wanafunzi wa mwaka wa kwanza kusaini malipo ya fedha hizo
Serikali ya Tanzania, kupitia kwa Abul-Razaq Badru, Mkurugenzi wa Bodi ya Mikopo ya Elimu ya juu (HESLB) imetangaza kutoa mikopo kwa wanafunzi 21,500 tu kati ya 88,000 wa mwaka wa kwanza, sawa na asilimia 24.4 ya walioomba mikopo hiyo mwaka wa masomo 2016/2017.
Serikali pia imeanzisha utaratibu mpya wa kutoa fedha za kujikimu kwa mwanafunzi kulingana na asilimia yake ya mkopo. Mfumo ambao umesababisha baadhi ya wanafunzi kupewa Sh. 350/= kama fedha ya kujikimu kwa siku, tofauti na mwaka jana ambapo wanafunzi wote wenye mikopo walikuwa wakipewa Sh. 8,500/= kwa siku.
Erasmi Leon, Rais wa DARUSO, akitoa msimamo wa Serikali ya wanafunzi wa UDSM amesema wanapinga mfumo huo mpya wa HESLB na kwamba wanafunzi wa mwaka wa kwanza hawatasaini fedha hizo mpaka pale kasoro hiyo itakaporekebishwa.
“Kwa majina ambayo yameshatoka hakuna kwenda kusaini mpaka pale tutapowaruhusu na tutawaruhusu mara baada ya kufanikisha haki yenu. Nawasihi tuwe wamoja, tunaenda wawakilishi ili tusikilizwe na wajue tuna hoja gani.
Tuna kila sababu ya kusikilizwa na tukinyimwa nafasi tutaenda tukiwa wengi zaidi. Tutakapowahitaji muda wowote, kwa lolote naomba tushirikiane, twende pamoja, tusimame na tumalize pamoja kuhakikisha tunapata 8,500/= kwa kila mwanafunzi kama fedha ya kujikimu kwa siku,” amesema Erasmi.
Alikuwa akiwahutubia wanafunzi wa mwaka wa kwanza huku akitangaza uamuzi wa kuwachukua baadhi ya wanafunzi na kwenda makao makuu ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ikiwa ni hatua yao ya kwanza ya kutafuta suluhu kabla ya kuchukua uamuzi mkubwa zaidi.
Kwa upande wake Kasunzu Eliudi, Waziri wa Mikopo DARUSO, ameieleza *MwanaHALISI Online* kuwa, utaratibu mpya wa serikali utafuta ndoto ya maelefu ya wanafunzi kupata elimu ya Chuo Kikuu.
“Hatuwezi kukubaliana na uonevu huu, watoto wa masikini hawataweza kuendelea na masomo, wanapewa mpaka Sh. 500/= ya chakula na malazi kwa siku. Elimu ndiyo chimbuko la ukuaji wa sekta zote, lazima serikali iwekeze, kuwatelekeza wanafunzi ni kulitelekeza taifa,” amesema.
Mpaka sasa serikali imetoa mikopo kwa wanafunzi 11,000 tu nchi nzima na imeahidi kuongeza wanafunzi 10,500 katika awamu nyingine ili kufanya idadi kamili ya waliopewa mikopo ifikie 21,500 tu kati ya 88,000 walioomba mikopo.
Hata hivyo licha ya kutangaza kutoa mikopo kwa wanafunzi 3,996 kati ya 8,000 wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, HESLB imepeleka majina 949 tu chuoni hapo jambo linalosababisha wanafunzi wengi washindwe kujisajili na kuanza masomo.
“Wanafunzi wamezagaa tu, hawajui pa kwenda na hawana fedha za kujikimu mpaka sasa. Wamekuwa kama kuku waliopotea banda lao huku giza likizidi kutanda,” amesema Kasunzu.
Mpaka tunaenda mitamboni, msafara wa wanafunzi wa UDSM ukiongozwa viongozi wa serikali pamoja na wawakilishi wa wanafunzi wa mwaka wa kwanza walikuwa wamefika wizara ya elimu huku wakikwama kuonana na Waziri Profesa Joyce Ndalichako.
“Tumeambiwa Waziri na Naibu wote hawapo, sisi tunahitaji kuzungumza na mtu anayeweza kufanya maamuzi na tunataka kwenda Ofisi ya Waziri Mkuu ingawa kwa sasa Katibu wa wizara ya Eimu ametuomba tuzungumze na yeye kwanza,” amesema Boniface Emmanuel, Waziri Mkuu wa DARUSO.
Wakati fukuto hili likiendelea UDSM na hatima yake ikiwa bado haijajulikana, taarifa ambazo bado hazijathibitishwa zinasema kuwa Ijumaa ya kesho Rais John Magufuli atakuwa mgeni rasmi katika sherehe ya maadhimisho ya miaka 55 ya chuo hicho.