Baadhi ya wanawake wa Kitanzania
waliofungwa katika magereza ya China na Hong Kong, walishika ujauzito
kama moja ya mbinu ya kupitisha dawa za kulevya bila kugundulika kwenye
viwanja vya ndege na mipaka mingine ya kimataifa. Mwananchi limebaini.
Watanzania wanne walio katika magereza
ya China na Hong Kong walijifungua watoto kwa nyakati tofauti wakiwa
wanatumikia vifungo na wamekiri kuwa walibeba ujauzito kama mbinu ya
kupitisha dawa hizo bila kukaguliwa.
Watoto wanaozaliwa magereza baada ya
kufikisha mwaka mmoja hupelekwa katika vituo vya watoto yatima na
kusomeshwa na Serikali ya China hadi pale wazazi wao watakapomaliza
adhabu.
Imebainika kuwa watoto wawili wapo
katika vituo hivyo, mmoja tayari yupo Tanzania baada ya bibi yake
kumrejesha na mwingine bado yupo gerezani na mama yake.
Wanawake hao ambao wote wana umri wa
kati ya miaka 20 na 30 walieleza masikitiko yao jinsi ambavyo
wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya wanavyowarubuni ili kubeba
dawa hizo kwa ahadi za kuwapa fedha nyingi.
“Tunapata mimba makusudi kwa sababu
tulijua kuwa katika viwanja vya ndege vingi wajawazito hawakaguliwi hasa
wakiwa na mimba kwa hiyo tungebeba unga na kuupeleka China, halafu
baadaye tungerudi nchini na kutoa mimba au tukiamua tunajifungua,”
alisema mmoja wa wafungwa hao.
Hata hivyo, mbinu hiyo ilifanikiwa
katika Uwanja wa Ndege Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), lakini
haikufua dafu katika viwanja vya ndege vya China, Hong Kong, Macau na
Guang Zhou.
Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI),
Kamishna Diwani Athuman alisema hana taarifa za Watanzania hao lakini
ofisi yake inafanya taratibu za kuwasiliana na China ili kujua hali za
wanawake hao.
Mkurugenzi wa JNIA, Moses Malaki alisema
kwa kawaida kila mtu hukaguliwa kwa uangalifu bila kujali mjamzito au
la. Akielezea namna wanavyopimwa, Malaki alisema kwanza kila msafiri
hupimwa kwa mashine ya kawaida ambayo hubaini uwepo wa kifaa chochote
kisichotakiwa mwilini kwa mfano chuma kama hereni, bangili, mikanda
lakini si ndani ya tumbo.
“Iwapo mashine ya awali itatoa mlio hata
baada ya msafiri kutoa vitu vya chuma, basi atatakiwa kwenda katika
chumba maalumu cha ukaguzi wa mikono,” alisema.
Kamanda wa kitengo cha Polisi cha Dawa
za Kulevya, (SACP), Godfrey Nzowa alisema wapo wanawake kadhaa raia wa
Zambia, Zimbabwe, Nigeria, Afrika Kusini na Malawi ambao wamefungwa
katika magereza ya Tanzania kwa kusafirisha dawa za kulevya wakitumia
mbinu hiyo ya ubebaji wa mimba.
Alisema mbinu hizo zinatumiwa na
wanawake kwa sababu wajawazito hawakaguliwi kwa mashine za x-ray na
kwamba wengi walikamatwa kutokana na taarifa za kikachero.
7 Jan 2015
New
Njia mpya za kuvusha madawa ya kulevya zagunduliwa
mulo