IPO misemo mingi ambayo huashiria
kutokea kwa jambo liwe nzuri au baya, moja ya misemo hiyo ni ule usemao
dalili ya mvua ni mawingu.
Msemo huu unaweza ukawa na na maana kubwa hivi sasa kwa golikipa wa timu ya Dar es salaam Young African, Juma Kaseja ambaye hivi sasa inaonekana hana mawasiliano mazuri na uongozi wa timu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Twiga na Jangwani jijini Dar es salaam.
Mchezaji huyo mwenye heshima kubwa nchini mwishoni mwa mwaka uliopita aliachwa katika kikosi cha timu hiyo kilichoelekea visiwani Zanzibar kushiriki michuano ya mapinduzi, lakini isitoshe jina la Kaseja halijaonekana kwenye orodha ya wachezaji wa timu hiyo iliyotumwa shirikisho la soka barani Afrika CAF kwa ajili ya ushiriki wa kombe la shirikisho.
Matukio hayo yote yameibua maswali mengi kwa wapenzi na mashabiki wa timu hiyo juu ya hatma ya mlinda mlango huyo, hatua iliyotufanya tumtafute afisa habari na mawasiliano wa klabu hiyo Jerry Muro kutaka kufahamu kinaga ubaga kinachoendelea kati ya Kaseja na Yanga..
Muro amesema Kaseja kutohusishwa katika kikosi kilichopo Zanzibar na kilichotumwa CAF ni kujitakia mwenyewe.
“Ni vizuri tukianza kuwakumbusha wapenzi wetu tulipotoka tulipo na tunapoelekea na mimi nilipoingia nililikuta hili tatizo lipo na tulipoamua kulifuatilia na kulipatia ufumbuzi, lazima tuseme ukweli na kweli itatuweka huru, matatizo ya Juma Kaseja na Yanga yalisababishwa na yeye mwenyewe alipoona hana kipaumbele na Yanga”.
Na hii ilitokana na kutokupangwa mara kwa mara katika michezo mingi ya Yanga tofauti na zamani watu walivyokua wakimuelewa kama kipa bora Tanzania, lakini kwa mabadiliko ambayo klabu imekua ikipitia kwa namna moja na kwa mahitaji ya timu labda yalikua hayamfurahishi Juma kama binadamu’’ alisema.
Muro ameendelea kusema kwamba “ndani ya uongozi wa yanga benchi la ufundi liliamua kumtumia Dida kutokana na uwezo wake jambo ambalo Juma hakupata nafasi kutokana na mahitaji ya timu hali iliyopelekea baadhi ya mashabiki kulalamika kwa nini hapangwi”
“Lakini tuweke kumbukumbu zetu vizuri Kaseja kapangwa mechi ya Mtibwa kafungwa magoli mawili, kachezeshwa mechi dhidi ya CDA ya kirafiki na nyingine kule Shinyanga, pia ikumbukwe wakati Juma yupo Simba na hata na Yanga alikuwa anapangwa michezo yote hadi ya kirafiki, mbona wenzake hawakulalamika hadi kuamua kuondoka?
“ Lakini kwanini watu wanahoji kipindi hiki ambacho klabu imeamua kuinua vipaji na kutafuta watu wengine wa kuchukua nafasi ya Juma …? Aliuliza Muro, na kuongeza huo ndio mgogoro na Juma na sio wa maslahi…
Kuhusiana na kutoonekana mazoezini Muro amesema juma alipoona hapewi nafasi akaamua mwenyewe kuacha kuhudhuria mazoezi na tatizo hili lilianza taratibu.
“Ghafla Juma akasema haji mazoezini kwa sababu anaidai Yanga mara akageuka akaandika barua akasema hana matatizo na Yanga, mara mwanasheria wake akatuandikia barua ya masuala ya kisheria”
Hata hivyo, Muro amesema kuhusu ni lini Juma hajafika mazoezini aulizwe mwenyewe lakini kama hafanyi kazi hakuna atakacholipwa na wanataratibu zao.
“Hata kama una mkataba haufanyi mazoezi haulipwi na hili hatupepesi macho kama hatuna taarifa zako kutoka kwa mwalimu au daktari wa timu hatujui kuhusu mambo yako ya familia huji mazoezi hulipwi chochote na hatulipi chochote”.
Huo ni upande wa Yanga ambayo bado ina mkataba na Kaseja, mchezaji mwenyewe anasemaje! Juhudi za kumtafuta Juma Kaseja zinaendelea.