ALIYEKUWA Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Mara kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Bi.Esta Bulaya ambaye juzi alitangaza kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), amepata mapokezi makubwa Mjini Bunda jana akitokea jijini Mwanza akiwa na viongozi wa CHADEMA mkoani humo na Kanda ya Ziwa.
Akiwahutubia wananchi katika Viwanja vya Stendi ya Zamani, Bi.Bulaya aliwapongeza wananchi kwa mapokezi makubwa waliyompa na kumlipua mbunge wa jimbo hilo aliyemaliza muda wake, Bw. Stephen Wassira akisema muda wake wa kukaa serikalini unatosha.
Alisema katika Serikali ya Awamu ya Tano, viongozi kama Bw. Wassira hawafai kwani amekuwa Waziri muda mrefu lakini jimbo hilo bado halina maendeleo yaliyotarajiwa na wananchi.
"Wazazi wangu mimi ni mwanachama wa CCM na mimi nimekulia ndani ya chama hicho hivyo mkiona nimekimbia, mjue mambo yamenifika shingoni, katika mkoa huu kuna rasilimali nyingi ambazo hazijatumika vizuri ili ziwaondolee wananchi umaskini," alisema.
Akizungumzia uwazi na uwajibikaji, alisema viongozi wengi wa CCM hawataki kuwatetea wananchi na kushindwa kuwasimamia watendaji wa Serikali akitolea mfano mradi mkubwa wa maji mjini humo ambao umechukua miaka tisa bila Bw.Wassira kuukamilisha.
"Leo hii Wassira atakuja na sera gani kwa wananchi wakati ameshindwa kutekeleza wajibu wake kama mbunge na kiongozi wa Serikali, tuwakatae viongozi wa ngazi zote wanaotokana na CCM," alisema.
Aliongeza kuwa, umefika wakati wa majimbo yote mkoani humo kuchukuliwa na wagombea wa CHADEMA ambao watatimiza ahadi zao kwa wananchi na kutatua kero walizonazo.
Bi.Bulaya aliweka wazi dhamira yake ya kuwania ubunge wa Bunda Mjini kwa tiketi ya CHADEMA ambapo leo atashiriki kura ya maoni ya kumpata mgombea ubunge wa jimbo hilo kwa tiketi ya CHADEMA.
Naye mbunge wa Kahama, Bw. James Lembeli, alidai kuchoshwa na ufisadi uliopo ndani ya CCM na kuwataka wananchi wakubali kuiunga mkono CHADEMA kwa kuwaweka madarakani na kushika dola katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 25, mwaka huu.
Mbunge wa Musoma Mjini, Bw. Vicent Nyerere, alilitaka Jeshi la Polisi kutoa ushirikiano katika Uchaguzi Mkuu na kuacha kuitetea CCM huku akidai jeshi hilo ni sehemu ya Watanzania ambao wote wamepigika.