Wanachama CCM Zanzibar wakataa kumuunga mkono Lowassa - MULO ENTERTAINER

Latest

2 Aug 2015

Wanachama CCM Zanzibar wakataa kumuunga mkono Lowassa

Wanachama wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar, wamesema hawapo tayari kumuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, kwa kitendo cha kukihama chama hicho na kujiunga na Chadema.
 
Wametoa tamko hilo jana mbele ya waandishi wa habari katika ofisi kuu za CCM Kisiwandui.
Akitoa taarifa hiyo kwa niaba ya wanachama wezake, Katibu wa mkoa wa mjini CCM, Muhammed Nyawenga, alisema Lowassa asidhani kuwa wanachama wengi wa CCM walimuunga mkono wakati alipotangaza nia ya kugombea urais wa Muungano kupitia chama hicho, akadhani kuwa na sasa watakuwa pamoja naye.
Alisema wanachama wa CCM hususan kutoka Zanzibar wanachoangalia kwanza ni chama na mtu baadae hivyo kama kaamua kujiunga Chadema hawako pamoja naye.
“Tunamwambia Lowassa kama mvuvi wa pweza basi tutakutana mwambani,”alisema kupitia tamko hilo.
Walisema wanashangazwa na baadhi ya vyama vya upinzani hasa vile vinavyouunda Ukawa namna wanavyoendelea kuendesha siasa za ubabaishaji na ulaghai kwa Watanzania.
Alisema ni jambo la aibu na la kufedhehesha kuona kwamba hata baada kufikisha umri wa miaka 23 tangu kuanzishwa rasmi kwa vyama vya upinzani bado vyama hivyo vimeshindwa kuandaa wagombea wenye uwezo wa kuwaongoza Watanzania na kuishia kudaka mapumba yanayotoka CCM.
Alisema uamuzi wa Lowassa kutoka CCM sio jambo la kukishtua chama, wanachama wala viongozi wa chama hicho na kamwe CCM haiwezi kudhoofika wala kupasuka kwani sio mara ya kwanza kwa CCM kuondokewa na kiongozi muandamizi na kujiunga na upinzani.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa mjini Magharibi ambae alikuwa kinara katika kumuunga mkono Lowassa wakati akiomba ridhaa ya chama hicho kugombea urais kupitia CCM, Borafya Silima Juma, alisema kiongozi huyo anapenda madaraka na ukubwa na ndio maana baada ya jina lake kutopita ameamua kujiunga na Chadema.