Vyama vya Upinzani Zanzibar Vyagawanyika...Vimetofautiana Kuhusu Uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Zanzibar (ZEC) - MULO ENTERTAINER

Latest

8 Nov 2015

Vyama vya Upinzani Zanzibar Vyagawanyika...Vimetofautiana Kuhusu Uamuzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Zanzibar (ZEC)


Vyama vya upinzania kisiwani Zanzibar vimetofautiana kuhusu uamuzi wa mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu kwa maelezo kuwa haukuwa huru na haki.

Jana Chama Cha ACT-Wazalendo kiliunga mkono chama cha CUF, kupinga uamuzi huo wa Mwenyekiti wa ZEC.

Akiongea na waandishi wa habari visiwani humo, Makamu mwenyekiti wa ACT-Wazalendo, Ramadhani Suleiman alisema kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na haki kama ulivyoshuhudiwa na waangalizi wote wa ndani na nje ya nchi na kuitaka Tume hiyo kuendelea na zoezi la kuhakiki matokeo na kumtangaza mshindi.

Wakati huohuo, vyama vya CCK, TLP na SAU wao kwa pamoja walijitokeza na kuunga mkono uamuzi uliofanywa na mwenyekiti huyo wa ZEC wakidai kuwa uchaguzi huo ulikuwa na ukiukwaji mkubwa wa taratibu na kasoro nyingi zilibainika hasa katika visiwa vya Pemba.

“Tunaunga mkono kauli iliyotolewa na mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar, ya kufuta matokeo ya uchaguzi huo kutokana na vikwazo ambavyo Tume hiyo ilikabiliana navyo katika uendesha uchaguzi huo,” alisema mmoja kati ya wawakilishi wa vyama hivyo.

Mwenyekiti wa ZEC alitangaza kufuta matokeo ya uchaguzi huo muda mfupi baada ya mgombea wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kutangaza kuwa amekusanya matokeo ya vituo vyote na kubaini kuwa yeye ndiye mshindi huku akiitaka Tume hiyo kumtangaza.

Uchaguzi huo ulishuhudiwa kuwa na wagombea wa urais 14 lakini wagombea wawili, Maalim Seif Sharif Hamad (CUF) na Rais wa sasa, Dkt. Ali Shein (CCM) ndio waliokuwa na ushindani mkubwa zaidi.