Afanyayo Magufuli Siyo Mizani na Kumkomoa Kikwete ni Wajibu Wake - MULO ENTERTAINER

Latest

6 Jan 2016

Afanyayo Magufuli Siyo Mizani na Kumkomoa Kikwete ni Wajibu Wake

Wale watu wenye umri mkubwa wanajua kuwa Rais wa Kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere alikuwa na uhusiano mbaya na Shirika la Fedha la Dunia IMF na Benki ya Dunia akiwa madarakani.

Alipoingia madarakani, Ali Hassan Mwinyi aliamua kufuata masharti yaliyowekwa na mkubwa huyo. Hali ya uchumi ikawa mbaya. Hata hivyo, Mwalimu aliwafanya Watanzania kuwa kitu kimoja.
Mzee Mwinyi enzi hizo alipolaumiwa na baadhi ya watu akasema kwamba ‘kila zama na kitabu chake.” Nyerere hakuwa mkamilifu kwa asilimia 100, Mwinyi na Benjamin Mkapa vivyo hivyo.
Bila shaka, Jakaya Mrisho Kikwete naye si malaika na alikuwa na upungufu wakati wa miaka 10 ya utawala wake. Ukosoaji wowote dhidi ya Kikwete unakubalika ingawa nitatofautiana na kinachoendelea sasa .

Kwanza, wakosoaji wa Kikwete wanafanya hivyo kwa kumlinganisha na Magufuli jambo ambalo ni kosa kwa sababu Magufuli alikuwa na maono yake wakati akitaka urais na anayofanya sasa ni wajibu wake na ni kile anachokiona ni sahihi kwa taifa letu kusonga mbele. Kama kila anachofanya kitatafsiriwa kuwa ni kijembe dhidi ya mtangulizi wake, basi hilo ni kosa.

Tangu wakati wa kampeni, Magufuli alionesha dalili ya kuwa hivi alivyo. Wakati CCM kikimpa tiketi ya kuwania urais, kilijua kinampa mtu wa namna gani, kilijua atakuwa mkali kwa wavunja sheria na alikuwa akisema hilo waziwazi.

Katika hali ya kawaida, si rahisi kwa mtu kuelewa kwa nini Kikwete alikuwa na baraza la mawaziri la watu 60 kwenye awamu yake ya kwanza ya urais. Tukumbuke kuwa aliingia madarakani wakati kukiwa na mpasuko uliosababishwa na kundi la mtandao lililomsaidia aingie madarakani.
Hivyo basi, Kikwete fikra yake ya kwanza baada ya kuwa rais ilikuwa ni kuhakikisha kuwa kila kundi ndani ya chama linawakilishwa ndani ya serikali yake.

Jakaya-Kikwete2Niwakumbushe kuwa hata Nyerere wakati anaunda serikali ya mwanzo alihakikisha baraza la mawaziri linakuwa na Waafrika, Wazungu, Wahindi, Waislamu, Wakristo, yaani walau kila kundi la kijamii.

Magufuli alipoteuliwa kupeperusha bendera ya CCM kwenye kuwania urais alikuta chama kimeungana dhidi ya mgombea wa upinzani, Edward Lowassa.

Rais Magufuli ana historia tofauti na JK. Yeye ametokea kwenye taaluma ya ualimu. Kazi kubwa ya mwalimu ni kuhakikisha anamsaidia mwanafunzi kufikiri hadi kufikia mwisho wa uwezo wake wa kiakili kwa kushauri, kuelekeza, ukali na kadhalika na ndivyo anavyofanya sasa.

Naamini Magufuli atafanya kila analoweza kuhakikisha Tanzania inafikia anapofikiria kufikia na ili kufika hapo, atatumia kila aina ya mbinu alizojifunza kama mwalimu na pia kama mwanasiasa mkongwe kwani alikuwa waziri kwa miaka 20.

Kutokana na ukweli huo ndiyo maana, sioni busara ya kuwafananisha Magufuli na Kikwete kwa kuwatia kwenye mizani. Tukumbuke kuwa Kikwete aliikuta Tanzania ikiwa moja na akaiacha ikiwa moja na alikuwa karibu na wananchi wake na aliwapenda.

Ili kumsaidia Magufuli katika ndoto zake ni vema kila Mtanzania kueleza yalipo matatizo kwa kutumia njia yoyote, hilo litatusaidia kututoa hapa tulipo.
Jipu limepasuka, siwezi kuwa adui kwa kusema ukweli.